Murang’a yaibuka kitovu cha siasa Mlima Kenya
NA MWANGI MUIRURI
KAUNTI ya Murang’a imeibuka kuwa miongoni mwa ile inayovutia ubabe mkubwa wa kisiasa baina ya Naibu Rais Dkt William Ruto na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, wote ambao wanalenga kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.
Gatuzi hilo linajivunia zaidi ya wapigakura 600,000 na linaonekana kama kiingilio kwa mwaniaji yeyote anayetaka kura za Mlima Kenya.
Kinara wa ANC, Bw Musalia Mudavadi, alitambua hilo wakati aliendeleza kampeni zake za kusaka uungwaji mkono Mlima Kenya.
“Nipewa jina Macharia kwa sababu natambua kuwa, mwaniaji urais ambaye ameidhinishwa Murang’a mwishowe huungwa mkono na wakazi wa kaunti nyingine za Mlima Kenya,” alisema Bw Mudavadi miezi kadha iliyopita.
Vilevile, Seneta James Orengo wa Siaya akiwa kwenye ziara ya Mt Kenya pamoja na Bw Odinga, alisema wana uhakika kuwa iwapo waziri mkuu huyo wa zamani atapata kura za Murang’a basi atapigiwa kura na maeneo mengine.
Kihistoria, kaunti hiyo inazingatiwa kama asili ya jamii ya Agikuyu. Gikuyu na mkewe Mumbi walikuwa wakiishi eneo la tambiko linalopatikana eneobunge la Kiharu.
Mumbi alijifungua watoto tisa ambao ni sehemu ya jamii toto za Agikuyu.
Umuhimu wa eneo hilo la tambiko ulidhihirika wazi baada ya uhasama kutokea baina ya Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na Gavana Mwangi Wa Iria, baada ya Spika kutawazwa na wazee kadha kama msemaji wa jamii ya Agikuyu.
Bw Wa Iria alidai kuwa wazee hao walikosea na hivyo eneo hilo lilifaa kutakaswa kwani waliomtawaza Bw Muturi hawakuwa wakitambuliwa na uongozi wa Baraza la Wazee wa Agikuyu.
Kisiasa, Bw Odinga na Dkt Ruto wanaonekana kuwa na uungwaji mkono sawa wa viongozi wa hapo waliochaguliwa.
Wanaounga mkono mrengo wa Bw Odinga ni Wangari Mwaniki (Kigumo), Peter Kimari (Mathioya), Muturi Kigano (Kangema) na Nduati Ngugi (Gatanga).
Nao Ndindi Nyoro (Kiharu), Alice Wahome (Kandara) na Mary wa Maua (Maragua) pamoja na Seneta Irungu Kang’ata wanashabikia ule wa Dkt Ruto.
Bw Odinga na Dkt Ruto huenda wakawatoa wagombeaji wenza kutoka kaunti hiyo.
Katika kambi ya Dkt Ruto, Bi Wahome anadaiwa kuwa mstari wa mbele; huku Bw Odinga, akimnyemelea, mbunge wa zamani wa Gatanga Peter Kenneth.
Bw Wa Iria na mfanyabiashara Jimmy Wanjigi ambao pia wanawania urais, wanatoka Murang’a. Wanasiasa wakongwe walioshiriki ukombozi wa pili Charles Rubia na Kenneth Matiba pia wanatoka eneo hili.
“Sisi tunaopigia debe Raila tumepanga mikutano mingi ya kisiasa na wakati ambapo tutamaliza, uungwaji mkono anaojivunia Dkt Ruto,” akasema Elias Mbau, Maragua.
Kando na Bw Odinga na Dkt Ruto, Bw Wa Iria na mfanyabiashara Dkt Jimmy Wanjigi pia wanalenga urais na wanatoka katika eneo leo. Wanasiasa wakongwe, walioshiriki ukombozi wa pili Charles Rubia na Kenneth Matiba pia wanatoka Murang’a