Museveni ataka Afrika ipiganie vikali viti viwili UN
NA AGGREY MUTAMBO
KAMPALA, Uganda
RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni, amezitaka nchi za Afrika kutokubali chochote kingine kutokana na mageuzi ya Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu Usalama hadi bara hili litakapopatiwa angalau viti viwili vya kudumu.
Akizungumza Alhamisi katika kikao na kundi la mawaziri wa kigeni kutoka kote barani, kiongozi huyo wa Uganda alisema Afrika, sawa na maeneo mengine yanayoendelea duniani, hawaombi kupendelewa wanapoitisha kuwakilishwa kikamilifu.
Alisema, ni “dhahiri” kwamba mageuzi hayo yatafanya shirika hilo kuwa na ujumuishaji unaofaa.
Alisema haya wakati mawaziri kutoka mataifa 10 ya Afrika waliotwikwa jukumu la kupigia debe matakwa ya Afrika kuhusu mageuzi, walipokamilisha mkutano jijini Kampala wakitoa wito wa kutolegeza kamba kuhusu matakwa hayo.
“Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu Usalama lilipaswa na ni sharti lifanyiwe mageuzi. Hili si ombi la kumpendelea yeyote bali haki ya watu wote wanaoishi katika sayari ya dunia,” alieleza halaiki ya watu katika Hoteli ya Commonwealth Speke Resort mjini Munyonyo, Kampala.
Mawaziri waliokusanyika Kampala wanatoka mataifa 10 yaliyoorodheshwa na Umoja wa Afrika kama C-10, au Kamati ya 10.
Wanatoka Kenya, Uganda, Senegal, Zambia, Sierra Leone, Congo-Brazzaville, Libya na Namibia.
Nchi hizi kwa pamoja, chini ya mwenyekiti wake Sierra Leone, zimekuwa zikikusanya maoni kutoka kwa mataifa wanachama na wadau wengineo kote duniani tangu 2015 katika juhudi za kuwezesha mabadiliko katika Baraza hilo.
Hamu ya kufanyia mabadiliko Baraza la UN kuhusu Usalama, ambalo ni shirika lenye nguvu zaidi la UN imekuwa ikichochewa na Afrika na mataifa mengine kwa karibu miongo miwili sasa.
Bara la Afrika linahoji kuwa Baraza hilo lenye wanachama watano wa kudumu walioteuliwa wakati lilipobuniwa na wanachama 10 wasio wa kudumu limejitenga na uhalisia.
UN ilipobuniwa mnamo 1945, mataifa hayo matano ambayo sasa ni wanachama wa kudumu wa Baraza la UN kuhusu Usalama yalikuwa na uchumi thabiti, yalikuwa yameibuka washindi baada ya Vita Vya Pili vya Dunia au yalikuwa na idadi kubwa ya watu.
Mataifa hayo matano ni Amerika, Uingereza, Urusi, Uchina na Ufaransa.
Leo hii, hata hivyo, uchumi wa Ujerumani kwa mfano, umenawiri pakubwa kushinda wa Ufaransa na Uingereza na ulimwengu uliokuwa bado ukitawaliwa na wakoloni wakati huo umepata uhuru na kuanza kujitawala.
Wakati huo huo, visa vya COVID-19 vimepungua pakubwa huku idadi ya vifo ikishuka Barani Afrika kwa mara ya kwanza tangu wimbi la nne la mlipuko wa virusi aina ya Omicron lilipofikia kilele, Umoja wa Mataifa umesema.
Afisi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inayosimamia Bara la Afrika ilitaja mkurupuko huo wa siku 56 Afrika kama ulio mfupi zaidi kufikia sasa.
Aidha, ilisema kuwa idadi ya visa vipya vilivyoripotiwa ilishuka kwa asilimia 20 kwa kipindi cha wiki moja hadi kufikia Jumapili huku idadi ya vifo vilivyoripotiwa ikipungua kwa asilimia nane.
Kupitia taarifa iliyotolewa baada ya hotuba ya kila juma, WHO ilisema vilevile kuwa Afrika Kusini iliyogundua kisa cha kwanza cha Omicron imeshuhudia kupungua kwa idadi ya visa katika kipindi cha mwezi mmoja.
Next article
WANDERI KAMAU: Polisi wachukue hatua na sio kupuuza maiti…