Mvurya adai mgomo wa madaktari umechochewa kisiasa
NA SIAGO CECE
MGOMO wa wahudumu wa afya katika Kaunti ya Kwale unatazamiwa kuendelea kwa wiki ya pili, na kusababisha shughuli za matibabu kutatizika baada ya serikali ya kaunti hiyo kutupilia mbali matakwa ya waajiri hao, ikidai mgomo huo umechochewa kisiasa.
Hata hivyo, Gavana wa Kwale Salim Mvurya lakini alisema marupurupu wanayodai wahudumu hao yatalipwa baadaye mwezi huu pamoja na mishahara yao.
“Ikiwa tumehakikisha kuwa tumewalipa wahudumu wa afya tarehe 24 ya kila mwezi bila kuchelewa, kwa nini wasiripoti kazini?” Bw Mvurya aliuliza.
“Najua huu ni mpango wa wapinzani wangu na wa Fatuma Achani kutufanya sisi viongozi kuonekana kama hatuwalipi wafanyikazi,” aliongeza.
Aidha alisema walikutana na wahudumu hao wa afya na kukubaliana kwamba marupurupu yanayodaiwa yatalipwa mwezi Februari 20, lakini bado watumishi hao waligoma kufuta mgomo huo.
Bw Mvurya alishikilia kuwa wahudumu wa afya wasioripoti kazini watafutwa kazi.
“Kuna kaunti nyingi sana ambazo unaweza kuzifanyia kazi na tutakufuta kazi ili uende. Huwezi kutumia siasa kujaribu kusema kuwa kaunti hii haiwalipi wafanyikazi wake,” akasema.
Alikuwa akizungumza katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kwale wakati wa uzinduzi wa kampeni ya chanjo katika kaunti hiyo. Bw Mvurya alisema Kwale imechanja asilimia 11 pekee ya wakazi wake, idadi ambayo bado ni ndogo.
Wakati huo huo, wahudumu wa afya wakiongozwa mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Wauguzi (Knun) tawi la Kwale Tobias Onyango walisema kwamba watarejelea tu kazi madai yao yote yatakapolangaziwa.
“Hakuna kitu kama siasa. Malalamiko yetu yote ni ya kweli na waajiri wetu wanapaswa kukubali hilo na kutulipa,” ameambia Taifa Jumapili kwenye mahojiano.
Haya yanajiri huku zahanati nyingi katika kaunti hiyo zikisalia zimefungwa huku zile chache zikiwa na wagonjwa wanaotatizika na kusubiri kwa muda mrefu kabla ya kutibiwa.