Sote tunajua sukari ni tamu na ni miongoni mwa bidhaa zinazotumika kwa wingi kila siku katika nyumba zetu. Lakini licha ya umuhimu wake, sukari ni hatari kwa ustawi wa afya wakati inapotumiwa kwa wingi kupita kiasi.
Kwa kawaida kiwango cha sukari tunachotakiwa kutumia katika vinywaji vyetu, iwe chai, juisi, na vinginevyo, ni kiasi kidogo sana, ila kwa upande mwingine, unapoweka sukari kiasi kidogo, ladha ya kinywaji au chakula hicho huonekana ni kama haijakamilika vyema.
Wakati tunapotafuta ladha ya sukari iliyokolea, baadhi yetu hupenda kuweka kiasi kingi kwenye vinywaji na vyakula vyetu na matokeo yake sisi hujikuta katika matatizo makubwa ya kiafya bila ya kujua kuwa chanzo ni sukari.
Bila shaka unaweza kujiuliza kiasi kingi cha sukari ni kipi? Mazoea yanaonyesha kuwa watu wengi huweka vijiko vitatu hadi vinne vya sukari kwenye kikombe kimoja cha chai wastani kama kiwango chao cha kawaida. Kiwango hicho hakika ni kingi mara nne ya kile kinachokubalika kiafya.
Kikombe wastani cha chai huhitaji kijiko kidogo kisichozidi kimoja na hata ikiwezekana pungufu ya hapo. Pia unashauriwa kujiepusha sana na unywaji wa vinywaji, kama juisi na soda ambavyo huongezewa sukari ya ziada.
Wataalamu wa afya wanatueleza kwamba chupa moja ya soda huwa na wastani wa vijiko sita vya sukari, kiasi ambacho ni kikubwa mno kuliko kawaida. Kwa hivyo ni vyema kujiepusha na unywaji soda kupindukia ukidhani unakunywa kinywaji salama kwa kuwa hakina kilevi.
Sukari inaweza kuepukika kweli?
Sio rahisi kuepuka kabisa matumizi ya sukari na kuiondoa katika milo yetu ya kila siku, lakini wakati mtu anapoelewa kuhusu madhara yake na lengo la kuiepuka ndipo atakapo kata shauri kupunguza kiwango anachotumia kwa siku.
Hapa ni baadhi ya vidokezi vinavyoweza kukusaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa matumizi ya sukari:
Fanya mazoea ya kusoma kiasi cha sukari kinachopatikana kwenye chakula au kinywaji chako. Mara nyingi kiasi cha sukari kinachowekwa kwenye kinywaji huoneshwa kwa gramu, ambapo kijiko kimoja kidogo cha sukari ni sawa na gramu 4. Hivyo ina maana kwamba iwapo kinywaji au chakula chako kina gramu 16 za sukari, hiyo ni sawa na vijiko vidogo vinne.
Wakati wote kuwa makini na chunguza kwa karibu, kwani vinywaji vingine havioneshi jina la sukari moja kwa moja, badala yake huiita kwa majina kama vile high fructose, molasses, dextrose, n.k.
Vilevile, ili kupunguza wingi wa sukari mwilini, unashauriwa kunywa kiasi kingi cha maji kila siku, na kuepuka unywaji wa pombe kupita kiasi. Aidha madaktari wanatushauri kupata muda wa kutosha wa kupumzika ama kulala.
Kwa kawaida kinga ya mwilini ni silaha ya asili ya mwili ya kupambana na maambukizi yoyote yanayosababishwa na bakteria, virusi na wadudu (parasites) wengine wanaobeba maradhi. Kwa kinga ya mwilini ya uhakika, ni muhimu kuimarisha kinga hiyo kwa kula vyakula vyenye virutubisho na kujiepusha na ulaji wa vyakula vyenye sukari ambayo mara nyingi huathiri mfumo mzima wa kinga hiyo.
Kuna ushahidi wa kutosha wa kisayansi kuwa matumizi ya sukari kupindukia huathiri mfumo wa kinga ya mwilini.
Seli nyeupe za damu (white blood cells) ndizo seli zinazoimarisha mfumo wa kinga ya mwilini, lakini kiasi kikubwa cha sukari kinapoingia kwenye damu, hudhoofisha uwezo wa seli hizo kupambana na magonjwa yanayoletwa na bakteria na virusi.
Baada ya kufahamu kwamba kinga ya mwilini ndiyo msingi wa afya bora ya binadamu, ni vizuri kujiepusha na matumizi ya vyakula ambavyo huenda vikahatarisha kinga yako ya mwilini. Na kila wakati ni lazima mtu kujiuliza kama matumizi yake ya sukari ni ya kiwango cha kawaida ama ni ya kuhatarisha afya yake, na kama matumizi hayo ni ya kuhatarisha, ni muhimu chukua hatua mara moja.
Makala yameandikwa na Daktari Ali Hassan, daktari binafsi, Nairobi.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.