[ad_1]
Mzozo wa urithi wa kisiasa Nandi watishia nafasi ya Sang 2022
Na TOM MATOKE
MZOZO wa kisiasa miongoni mwa viongozi wa Kaunti ya Nandi kuhusu madai ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya mali ya umma na siasa za urithi wa 2022 unaendelea licha ya Naibu Rais William Ruto kuingilia kati.
Naibu Rais anatazamiwa kuzuru kaunti hiyo kesho ili kuwapatanisha viongozi wa eneo hilo. Gavana wa kaunti hiyo, Stephen Sang amepuuzilia mbali madai ya wakosoaji wake kuwatimua wafanyikazi kutokana na mishahara duni huku akiwashutumu kwa kueneza siasa za kuwagawa wananchi.
Hata hivyo Bw Sang ameapa kuajiri wahudumu zaidi wa afya katika vituo vya kaunti ndogo ili kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya.“Ni kinaya kwamba baadhi ya viongozi ambao wametangaza nia ya kugombea nyadhifa mbalimbali ikiwemo ugavana wanazua taharuki miongoni mwa wafanyakazi kwa kutaka kufutwa kazi ili kupunguza mishahara yao.
Jambo hilo sitaliruhusu nikiwa uongozini,” akasema Bw Sang. Kadhalika, aliwakashifu viongozi wanaoshutumu utawala wake kwa rekodi duni za maendeleo. Wabunge sita wamekabiliana na Gavana Sang kuhusu miradi ya maendeleo iliyokwama na madai ya kukithiri kwa ufisadi katika utawala wake.
Wabunge hao ni Alfred Keter (Nandi Hills), Cornelly Serem (Aldai), Vincent Tuwei (Mosop), Julius Meli (Tindiret), Wilson Kogo (Chesumei) na Samson Cherargei (Seneta). Spika wa bunge la kaunti, Joshua Kiptoo na wakili, Allan Kosgey ambao wametangaza nia ya kuwania kiti cha ugavana wamemlaumu Bw Sang kwa madai ya kushindwa kubadilisha kaunti hiyo wakitaja bili kubwa ya mishahara kutokana na kuajiri ‘wafanyakazi hewa’.
[ad_2]
Source link