Namsubiri naibu wangu debeni – Lonyangapuo
NA OSCAR KAKAI
GAVANA wa kaunti ya Pokot Magharibi John Lonyangapuo amesema kuwa yuko tayari kukabiliana na naibu wake Dkt Nicholas Atudonyang kwenye kinyanganyiro cha ugavana wa kaunti hiyo.
Naibu huyo wa gavana ambaye alikuwa mafichoni aliwasili nchini wiki mbili zilizopita.
Ni Daktari wa upasuaji wa ubongo nchini Marekani na hajakuwepo kwenye kaunti hiyo kutoka mwaka wa 2018.
Dkt Atudonyang yuko tayari kupambana na mkubwa wake John Lonyangapuo kwenye uchaguzi mkuu ujao wa Agosti 9, 2022 katika chama cha Kanu.
Prof Lonyangapuo aliyeunda chama cha Kenya Union Party (KUP) alisema kuwa atamshinda mdogo wake huyo.
Prof Lonyangapuo alisema kuwa anaelewa vyema siasa na hamuogopi naibu.
Prof Lonyangapuo alisema kuwa wakazi wa kaunti ya Pokot Magharibi walipea Dkt Atudonyang nafasi ya kuwa naibu wa gavana lakini akaipuza.
“Alipewa nafasi kisha akaanza kukosa heshima na hata kupotea. Mimi ndiye kinara wa siasa na nilisomea hesabu halisi kutoka chuo kikuu cha Leeds. Mimi ndiye nilibeba viongozi wote ambao sasa wananipiga vita,” alisema.
Akiongea mjini Kapeguria wiki hii, Prof Lonyangapuo alisema kuwa Dkt Atudonyang hawezi kuaminika na wapigakura kwa kukosa kufanya maendeleo kwenye kaunti hiyo.
“Tumesikia kuwa unakuja, kuja haraka na fedha hizo na nitakuonyesha kivumbi kikali na hizo pesa zako,” alisema Prof Lonyangapuo.
Kwenye mahojiano na runinga ya Citizen wiki moja Jumapili iliopita, naibu wa gavana alidai kuwa amekuwa kwenye kaunti hiyo siku mbili zilizopita.
Alisema kuwa hajakuwa akipokea mshahara wake kwa miaka minne iliyopita kama njia ya kukata matumizi ya fedha.
“Nilisaidia kwa kupunguza fedha za matumizi. Mimi ni naibu wa gavana ambaye amefanya mengi kuliko wengine. Matumizi ya ofisi yangu yako chini sababu tuliajiri watu wengine na mshahara wangu. Serikali ya kaunti imeajiri maafisa 30,” alisema.
Alisema kuwa hakutaka kujiuzulu sababu ingeonekana kuwa mwenye ametoroka majukumu yake baada ya kupewa na wapiga kura wa kaunti hiyo.
“Kujiuzulu ingekuwa kana kwamba nimehepa majukumu. Sababu ya kuchaguliwa ni kandarasi kati yangu na mkubwa wangu na watu. Kuna njia ya kuangalia suala hilo. Watu walitosheka? Ninavyoona wako na furaha na kazi yangu kwenye ofisi. Walikuwa na nafasi ya kunibandua ofisini, lakini mmesikia kuhusu mimi kubanduliwa kweli?” aliuliza.
Akaongeza: “Hakuna wakati niliulizwa na gavana nifanye kazi na nikakosa. Nilifanya kila kitu niliambiwa nifanye. Sina shinda yoyote na yeye. Nina heshima na tumekuwa marafiki miaka hii yote.”
Alisema kuwa walifanya kazi hapo kwa hapo na gavana kabla ya kuenda Texas.
Hata hivyo alisema kuwa licha ya kutokuwepo alisaidia kupunguza matumizi ya fedha katika ofisi ya naibu wa gavana akijitetea kuwa amekuwa akifanya kazi vyema akiwa nje.
Alisema kuwa alifaulu kuongeza basari hadi milioni 400 kwenye kaunti.
Mwingine anayewania wadhifa huo ni aliyekuwa gavana Simon Kachapin kwenye chama cha United Democratic Alliance (UDA).
Next article
Mwaniaji urais sasa ahamia ELP kutoka Ford Asili