Connect with us

General News

NCPB yadumisha bei ya mahindi licha ya zao kujaa kutoka nje – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

NCPB yadumisha bei ya mahindi licha ya zao kujaa kutoka nje – Taifa Leo

NCPB yadumisha bei ya mahindi licha ya zao kujaa kutoka nje

NA BARNABAS BII

IDADI ya mahindi yanayowasilishwa na wakulima katika Halmashauri ya Kitaifa ya Ununuzi wa Nafaka (NCPB) imeongezeka maradufu katika muda wa majuma mawili yaliyopita.

Hii ni baada ya halmashauri hiyo kudumisha bei ya kununua gunia moja la kilo 90 za mahindi kuwa Sh3,000 licha ya kushuka kwa bei za zao hilo sokoni.

Kufikia sasa, halmashauri imenunua magunia 50,000 ya mahindi ikilinganishwa na magunia 20,000 mwanzoni mwa mwezi uliopita.

Bei ya kawaida ya zao hilo ilishuka kutoka Sh3,200 hadi Sh2,800 baada ya mahindi ya bei rahisi kuingizwa nchini kutoka Uganda na Tanzania.

“Tutaendelea kuwanunulia wakulima mahindi yao kwa Sh3,000 kwa gunia moja licha ya bei ya kawaida ya zao hilo kushuka,” akasema Bw Joseph Kimote, ambaye ndiye Mkurugenzi Mkuu wa halmashauri hiyo.

Alisema kuwa kiwastani, halmashauri inapokea magunia 3,000 ya mahindi kila siku.

Aliwarai wakulima kuwasilisha mahindi kwao, akiahidi kutochelewesha malipo yao.

Kushuka kwa bei ya mahindi ni pigo kubwa kwa wakulima, ikizingatiwa wengi wao wamekuwa wakilalamikia bei ya juu ya pembejeo.

Wasagaji wengi wamepunguza mahindi ambayo wamekuwa wakinunua kutokana na kupungua kwa kiwango cha unga kinachonunuliwa na wateja katika sehemu tofauti nchini.

“Wasagaji wengi wamelazimika kupunguza kiwango cha mahindi wanayonunua kwani hitaji lake limepungua kutokana na ongezeko la mahindi yanayoingizwa nchini,” akasema Bw Kipng’etich Mutai, ambaye ndiye mwenyekiti wa Chama cha Wasagaji cha Grain Belt Millers.

Wasagaji wameonya huenda bei za zao hilo zikapungua zaidi, baada ya wakulima katika baadhi ya sehemu za nchi kuvuna mazao ya msimu mfupi. Ni hali inayotajwa kuwaathiri sana wakulima, ikizingatiwa wengi wao wamekuwa wakilazimika kutumia fedha nyingi kwenye shughuli za upanzi na uvunaji.