Connect with us

General News

Ndege wa umaridadi wanampa tabasamu – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Ndege wa umaridadi wanampa tabasamu – Taifa Leo

Ndege wa umaridadi wanampa tabasamu

Na SAMMY WAWERU

ONESMUS Gitonga ni kijana ambaye kwa umri wake, anajivunia hatua alizopiga kimaendeleo kutokana na ufugaji wa ndege wa umaridadi wa nyumbani.

Ni safari iliyong’oa nanga mwaka wa 2017, baada ya kupoteza ajira katika nchi jirani ya Tanzania.

“Nilipopoteza kazi, nilitathmini jinsi ya kuwekeza fedha nilizokuwa nimekusanya,” Gitonga asema.

Anadokeza nyumbani kwao, Nanyuki, Kaunti ya Laikipia walikuwa na batamzinga wawili; wa kike na kiume, walioangua vifaranga 15, na ambao kulingana naye walifungua jamvi la ufugaji wa ndege wa umaridadi.

“Nilichapisha tangazo la mauzo kwenye makundi ya Facebook, ya kilimo na ufugaji na chini ya siku mbili vifaranga wote walikuwa wamenunuliwa,” anaelezea.

“Oda ziliendelea kumiminika licha ya wote kununuliwa.”

Anasema idadi kubwa ya wateja aliopata ilimchochea kuwekeza katika mradi wa batamzinga.

Aidha, mapato aliyotia kibindoni pamoja na akiba yake, alinunua batamzinga kadhaa wa kike, ili ‘kuwazalisha’.

Kulingana na masimulizi yake, oda alizoendelea kupata alizigeuza kuwa biashara ambapo alikuwa akinunua ndege kutoka kwa wafugaji na kuuza na kuvuna faida.

Ni kupitia mwanya huo kijana huyu alikuja kugundua kuna ndege wengine wa umaridadi wanaofugwa nyumbani kama vile; kuku aina ya bantam, bata na njiwa.

“Niliwajumuisha, na mradi ukaendelea kukua,” asema.

Spishi zisizopungua 20 kwenye mradi wake

Gitonga, akiwa na umri wa miaka 29 kwa sasa ndiye mmiliki wa (NesKi Ornamental Birds Farm), shamba lenye ndege wa umaridadi wasiopungua aina 20, lililoko eneo la Ruai, Marura, Nanyuki.

Anasema mahitaji ya ndege wa umaridadi anaofuga na ambao zamani walikuwa wamekumbatiwa na mabwanyenye pekee, yanaendelea kuongezeka kwa kile anataja kama “wenye mapato ya kadri kutambua umuhimu wao”.

Anaiambia Akilimali kwamba kufikia sasa ana kanga 30, bata aina ya Rouen 10, Pekin 17, wenye asili ya Kihindi 10, kuku wa rangi tofauti 20 na aina ya Brahma 8.

Mradi wa Gitonga hali kadhalika una booted Bantams 12, cochin Bantams 6, na gianta cochin 4.

Ndege wengine wa umaridadi ni pamoja na njiwa aina ya Fantal 12, Jacobin na Capuchini 6 kila spishi, mabatamzinga 20 na mabatabukini 25.

Onesmus Gitonga akionyesha batabukini. Picha/ Sammy Waweru

Mfugaji huyu wa aina yake anafichua kwamba kwa sasa anaendeleza mikakati kuzindua mradi mwingine katika taifa jirani la Tanzania, kwa sababu pia ana wateja wengi nchini humo na Uganda.

“Kiwastani, pea ya kanga huuza Sh5,000 thamani ya Kenya, booted bantams Sh7,000, na kuku wenye rangi tofauti kati ya Sh18,000 – 20,000,” anaelezea.

Pea ya bata aina ya Rouen huuza Sh7,000, njiwa aina ya Jacobin Sh40,000 na Capuchin Sh17,000.

Vilevile, huuza mayai ya ndege hao, la bei ya chini likiwa la Sh200, kulingana na spishi.

Idhini ya KWS kuruhusiwa kufuga

Gitonga anasema mitandao ya kijamii ndiyo majukwaa yake kusaka soko.

“Ukurasa wa Facebook, NesKi Ornamental Birds Farm, huutumia kutafuta wateja. Husambaza ndege kila kona ya nchi, na katika taifa la Tanzania na Uganda,” anafafanua, akithibitisha kwamba ana kibali kutoka kwa Shirika la Wanyamapori Nchini (KWS) kufuga ndege wa umaridadi.

Leseni, kwa ndege wanaohusishwa na KWS ni Sh1, 500 spishi za kwanza, kisha Sh500 katika kila spishi mfugaji anataka kuongeza.

Mahitaji mengine ni nakala ya hatimiliki au makubaliano ya kipande cha ardhi unachonuwia kuendeleza ufugaji, maelezo ya eneo, picha za vizimba, nakala ya kitambulisho cha kitaifa na pini ya Mamlaka ya Ushuru (KRA).

“Baada ya kuafikia matakwa hayo, afisa kutoka KWS atazuru eneo akague ili kuruhusiwa kuingilia ufugaji,” Gitonga adokeza.

Anasema changamoto kuu kuanzisha ufugaji wa ndege wa kurembesha mazingira ni ukosefu wa mtaji, kwa sababu nyuni hao hawapatikani kwa urahisi na ni bei ghali.

“Isitoshe, kila aina ya ndege wanahitaji vizimba au makazi yake kuepuka kujamiiana wenyewe kwa wenyewe, ambapo ni gharama kuyajenga,” aelezea, akidokeza kwamba makazi ya utangulizi yalimgharimu Sh11,000.

Ameyajenga kwenye kipande cha ardhi chenye ukubwa wa robo ekari.

Anasema siri kufanikisha ufugaji wa ndege wa umaridadi, ni kuzingatia na kudumisha kiwango cha usafi wanakoishi na katika mazingira yao.

“Nyuni wa umaridadi usipokuwa makini katika suala la usafi huhangaishwa na maradhi ya ndege. Hakikisha mazingira yake ni safi, chakula na pia maji na vifaa vya kuwalisha na kuwanyweshea maji,” anashauri.

James Muthua, mtaalamu anataja New castle, Homa ya Matumbo ya Fowl, Fowl pox, Salmonellosis, Kipindupindu cha Fowl, Coccidiosis, Marek na Avian influenza kama maradhi hatari kwa ndege.

“Usafi, na kuzingatia ratiba ya chanjo, matibabu ya haraka wanapoonyesha dalili za kuugua, ndio chanzo kufanikisha ufugaji ndege,” ashauri mdau huyu ambaye ni mwasisi wa Jaymaish Vet Care.

Kulingana na uzoefu wa Gitonga kufuga ndege hao, bata ni vigumu kuathirika na maradhi kwa sababu ya kinga yao kuwa juu.