ANASEMA kuwa amepania kujituma mithili ya mchwa huku akilenga kuibuka kati ya wanamaigizo tajika miaka ijayo. Ann Wanjiku Njoroge ama ukipenda Annita Patric anaorodheshwa kati ya chipukizi wanaolenga kutinga hadhi ya kimataifa ambapo amezamia uigizaji na uana mitindo.
Kisura huyu ni mwanafunzi wa mwaka wa pili anakosemea masuala ya ubunifu wa mavazi kwenye taasisi iitwayo East Africa Institute of Certified Studies (ICS College) jijini Nairobi. Dada huyu aliyetua duniani mwaka 1998 kando na uigizaji mwana mitindo wa kujitegemea.”Nilianza kushiriki masuala ya uigizaji muda tu baada ya kumaliza chuo mwaka 2018.
Kiukweli nilivutiwa na uigizaji tangia nikiwa mwanafunzi wa shule ya Msingi baada ya kutazama filamu za Kinigeria (Nollywood),” anasema na kuongeza kuwa anaamini ipo atawika na wafuasi wa burudani wamkubali. Katika mpango mzima ni chipukizi anayepania kupambana mwanzo mwisho kuhakikisha anatimiza azma yake kuibuka staa katika uigizaji kama Destiny Etiko mzawa wa Nigeria aliyeshiriki filamu kama Battle of Queens kati ya zingine.
Ndani ya kipindi cha miaka mitano analenga kuwa mwigizaji na mwana mitindo anayefahaika nchini. Kisura huyu anajivunia kushiriki vipindi kadhaa akishirikiana na mwigizaji Spuiro ambazo zinapatikana kwenye mtandao wa youtube.
Baadhi yazo zikiwa ‘How rich guys make ladies laugh with dry jokes,’ ‘Never trust ghetto girls,’ na ‘How mother in law behave when she doesn’t like you.’ Kuhusu kwa nini wapenzi wa burudani huvutiwa na filamu za waigizaji wa Kinigeria anasema katika taifa serikali inatambua tasnia ya uigizaji na imewekeza zaidi kinyume na ilivyo hapa nchini.
Ann Wanjiku Njoroge ama ukipenda Annita Patric…Picha/JOHN KIMWERE
Barani Afrika anasema angependa kufanya kazi na Chacha Ike Faani mzawa wa Nigeria aliyeingiza filamu kama ‘The outcast,’ ‘Acry for Justine,’ na ‘Beach 24,’ kati ya zingine. Hapa nchini angependa kushirikiana na wasanii kama NYCE ‘Shiro’ Wanjeri ameshiriki vipindi kama ‘Ithaka riene,’ na ‘Aunty Boss.’ Pia yupo Sarah Hassan anayefahamika kwa filamu alizoshiriki ikiwamo
‘Just in time Muthoni,’ na ‘Crime and Justice Detective Makena.’ Anadokeza kuwa anatamani sana kuanzisha brandi yake ya kuzalisha filamu ili kusaidia waigizaji wanaokuja.
Kwenye uana mitindo anajivunia kufanya kazi na Aftamath Modelling Agencies na Sauti Africa Modelling Agencies. Kama mwana mitindo anajivunia kushiriki tangazo lililopeperushwa kupitia Inooro TV kwenye kipindi cha Ikumbi ria withi.
”Ingawa imekuwa mtihani mgumu maana mimi ni mfupi ukweli wa mambo ningependa kuwa Miss World pia Miss Universe na nimepania kuzidi kujaribu bahati yangu,” akasema. Ingawa hajapiga hatua sio mchoyo wa mawaidha. Anashauri wenzie kuwa kwa chochote wanachofanya wajitume kwa udi na uvumba pia kujiaminia wanaweza.
Ann Wanjiku Njoroge ama ukipenda Annita Patric…Picha/JOHN KIMWERE