Nema yakiri Bahari Hindi yachafuliwa, hatua kuchukuliwa
NA WINNIE ATIENO
MAMLAKA ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (Nema), imekiri kufahamu kuwa kuna uchafuzi wa bahari katika Kaunti ya Mombasa, lakini ikaahidi kuwa kuna mikakati inayoendelezwa kuzuia tatizo hilo.
Afisa wa Nema mjini Mombasa, alisema Shirika la Usafi na Kusambaza Maji Mombasa (Mowasco), lilishapewa ilani likarabati mabomba ya majitaka na likome kumwaga uchafu baharini.
“Tunajua kuna uchafuzi lakini mabomba yanaendelea kufanyiwa ukarabati. Tunajua kuna majitaka ambayo humwagwa baharini ndiposa tulichukua hatua haraka kutafuta suluhisho la kudumu. Kazi inaendelea na tunaamini ifikapo Machi hili tatizo litakuwa limesuluhishwa,” akasema.
Mkurugenzi Mkuu wa Mowasco, Bw Abdirahman Farah, alisema mabomba yaliyokuwa yakitegemewa yanabadilishwa.
Mabomba hayo yaliyojengwa zamani yanaaminika hayawezi kustahimili idadi ya watu na idadi kubwa ya viwanda.
Wataalamu wa uhifadhi wa mazingira walikuwa wamelaumu Serikali ya Kaunti ya Mombasa kwa ulegevu wa kuboresha mabomba ya majitaka na kumwaga uchafu baharini.
Mkurugenzi wa shirika la utafiti wa baharini la Coastal Oceans Research and Development – Indian Ocean (Cordio) anayesimamia ukanda wa Afrika Mashariki, Dkt David Obura, alitoa wito kwa kaunti hiyo kukarabati mabomba yote ambayo yameharibika.
“Watu ambao hutumia maji ya baharini kwa shughuli mbalimbali, au viumbe vya baharini wako hatarini kuathirika na bakteria zinazopatikana katika maji machafu. Majitaka, uchafu kutoka viwandani na aina nyingine za taka hutupwa ndani ya bahari. Kuna uchafuzi na sehemu kadhaa baharini huonekana kubadili rangi,” akasema Dkt Obura.
Wakati Gavana Hassan Joho alipohutubia bunge la Kaunti mwaka wa 2020, alitoa hakikisho kwamba hatua zinachukuliwa kuboresha usafi wa mji huo ikiwemo ujenzi wa mabomba mapya.
Mwanaharakati wa kimazingira, Bw Silas Juma, alisema wamekuwa wakiokota uchafu mwingi unaoshukiwa kutoka hospitalini kila mara wanapofanya zoezi la kusafisha fuo za bahari.
“Unaweza tu kuwaza ni kiwango kipi kingine kiko ndani ya bahari na ufuoni ambapo huwa tunatembea bila viatu,” akasema Bw Juma.
Next article
Mbunge alaani hatua ya wakazi kuweka uchawi mbele kuliko…