TAHARIRI: Ni aibu kwa Haji na Kinoti kuwania ubabe raia wakilia
NA MHARIRI
MVUTANO wa ubabe baina ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji na mwenzake wa Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) George Kinoti katika siku za hivi karibuni umechukua mkondo hatari.
Hapo jana Jumanne, Bw Kinoti ametaka Bw Haji akamatwe kwa madai ya kutoa taarifa uongo na kughushi saini.Haya yanajiri Rais Uhuru Kenyatta na Inspekta wa Polisi Hillary Mutyambai wakiendelea kutazama tu huku wananchi wakikosa haki, nao wahalifu wakisherehekea.
Bw Kinoti kupitia kwa barua yake kwa mahakama ya Nairobi mnamo Jumatatu, anadai kuwa Bw Haji alijumuisha majina ya maafisa wawili wa DCI kwenye orodha ya watu waliohudhuria vikao vya kuandaa mwongozo kuhusu namna ya kukabili ugaidi na kuandika sheria ya kupambana na ufadhili wa ugaidi.
Bw Kinoti anasema kuwa maafisa wake hao hawakuhudhuria vikao hivyo vilivyofanyika kati ya Februari 21 na Machi 2022.
Uhasama wa majuzi kati ya wawili hao umechochewa zaidi na uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu mnamo Jumatatu wiki iliyopita ambapo maafisa wa polisi walipigwa marufuku kutayarisha na kutia saini hati za mashtaka.
Jaji Anthony Mrima alisema hati za mashtaka zilizoandaliwa na maafisa wa polisi ni haramu.
Tayari Bw Kinoti amepiga marufuku maafisa wake kuandikisha taarifa kutoka kwa washukiwa au kutoa ushahidi kortini, hatua ambayo inatatiza Wakenya kupata haki.
Msururu huu wa matukio sasa unatishia kuvuruga mfumo mzima wa upatikanaji wa haki nchini.
Cha kushangaza ni kwamba Haji na Kinoti wamekuwa wakifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa tangu wateuliwe kuhudumu katika ofisi zao.
Kwa mujibu wa Katiba, ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka nchini ndiyo huwasilisha ushahidi kortini kuthibitishia mahakama kwamba washukiwa wana hatia.
Kwa upande mwingine, afisi ya Mkurugenzi wa uchunguzi ya DCI nayo hufanya uchunguzi kisha kuandaa hati ambayo hupekwa kwa DPP kufanyiwa tathmini kabla ya hati ya mwisho ya mashtaka kuandaliwa.
Hii ina maana kwamba ili mfumo wa haki ufanye kazi bila hitilafu, ofisi hizi mbili lazima zifanye kazi kwa ushirikiano. Majukumu ya ofisi hizi mbili pia yameainishwa wazi katika Katiba.
Iwapo zipo tofauti za kibinafsi kati ya Haji na Kinoti, hazifai kuruhusiwa kuathiri mfumo wa upatikanaji haki.
Mzozo wa sasa umetumbukiza taifa katika hali ya sintofahamu. Wanaofaidi kwa sasa ni wahalifu ambao hawawezi kushtakiwa huku umma ukiumia.