Mwai Kibaki (1931-2022): Ni heshima za mwisho
NA LEONARD ONYANGO
RAIS Uhuru Kenyatta, Ijumaa aliongoza Wakenya kutoa heshima zao za mwisho kwa Hayati Rais Mstaafu, Mwai Kibaki katika uwanja wa Nyayo katika hafla iliyohudhuriwa na marais watatu na mabalozi wa nchi mbalimbali.
Maelfu ya Wakenya waliamka Ijumaa alfajiri na kuelekea uwanjani Nyayo jijini Nairobi kwa ajili ya ibada ya kumuaga Kibaki, lakini wengine waliwahi katika hifadhi ya maiti ya Lee kuona mwili wa Kibaki ukitolewa kuelekea Ikulu.
Uwanja wa Nyayo ulio na uwezo wa kubeba watu 30,000 ulijaa hadi pomoni kabla ya saa 2.00 asubuhi.
Safari ya kuelekea Ikulu ilianza saa 2.20 asubuhi baada ya familia ya Kibaki kukutana kwa dakika kadhaa katika mochari ya Lee.
Mwili wa Kibaki uliwasili katika Ikulu ya Nairobi saa 3:07 asubuhi ambapo ulikuwa kwa takribani dakika 30 na kisha kupelekwa uwanjani Nyayo kwa ajili ya ibada.
Kabla ya msafara huo kuwasili uwanjani Nyayo, maafisa wa polisi walikuwa wakigawa miavuli kutokana na hofu kwamba, huenda mvua ingenyesha na kuvuruga hafla.
Watu kadhaa walipoteza simu waking’angania miavuli ya bwerere.
Wachuuzi pia walitumia fursa hiyo kuvuna kutoka kwa Wakenya waliokuwa wakielekea uwanjani.
Familia ya Mzee Kibaki, ikiongozwa na mwanawe Jimmy, iliwasili katika uwanja wa Nyayo saa tatu na dakika hamsini (3.50) asubuhi.
Viongozi wa muungano wa Kenya Kwanza; Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula walikuwa miongoni mwa Wakenya waliofika mapema katika uwanja wa Nyayo kabla ya saa 3.00 asubuhi.
Marais Sahle-Work Zewde (Ethiopia), Salva Kiir (Sudan Kusini), Cyril Ramaphosa (Afrika Kusini) na Makamu wa Rais wa Tanzania, Philip Mpango, Waziri Mkuu wa Rwanda, Édouard Ngirente, makamu wa Rais wa Zimbabwe Constantino Chiwenga na Makamu wa Rais wa Uganda, Jessica Alupo na Rais wa zamani wa Malawi Joyce Banda walikuwa miongoni mwa viongozi wa kimataifa waliohudhuria ibada hiyo.
Kizaazaa kilitokea baada ya walinzi wa mwaniaji wa urais wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga na mkewe Ida, walipozuiliwa kuingia katika eneo la watu mashuhuri.
Mlinzi mmoja aliyekuwa amevalia suti yenye rangi ya kijivu alijaribu kuingia kwa nguvu lakini akakamatwa na kukatazwa.
“Usilete fujo hapa,” afisa mmoja akamfokea.
Inadaiwa kuwa maafisa wa usalama waliokuwa wakilinda lango la watu mashuhuri walikuwa wameagizwa kuzuia walinzi kutoingia ndani.
Rais Uhuru Kenyatta aliwasili uwanjani humo saa 4.26 lakini aliingilia eneo tofauti na mahali ambapo naibu wake alikuwa amesimama kumlaki.
Dkt Ruto alipofahamishwa kuwa Rais Kenyatta amewasili, alikimbia katika eneo hilo kumlaki lakini kiongozi wa nchi hakumsalimia kwa mkono.
Uhasama baina ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto pia ulijitokeza wakati wa kutoa hotuba.
Dkt Ruto alikaribishwa na Askofu Anthony Muheria wa Dayosisi ya Nyeri kuzungumza.
Baada ya Ruto kukamilisha hotuba yake, kwaya iliimba nyimbo kadhaa na kisha Askofu Muheria akaalika Rais Kenyatta kuzungumza.
Kwa kawaida, Naibu wa Rais ndiye hutwikwa jukumu la kumwalika Rais kutoa hotuba yake katika hafla za kiserikali.
Awali, Waziri wa Usalama Fred Matiang’i alikuwa ametangaza kuwa hafla hiyo ingeendeshwa na wanajeshi na viongozi wa Kanisa.
Uhasama baina ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto pia ulidhihirika Jumatatu katika majengo ya Bunge baada ya kiongozi wa nchi kukwepa kumsalimia kwa mkono naibu wake.
Hatua hiyo ya Rais Kenyatta ilishutumiwa vikali na wandani wa Dkt Ruto wakiongozwa na Seneta wa Elgeyo Kipchumba Murkomen na Seneta Maalumu Millicent Omanga.
Mwili wa Mzee Kibaki uliokuwa ukipelekwa katika uwanja wa Nyayo kwa gwaride ya kijeshi kutoka Ikulu uliwasili uwanjani humo saa 4.30 asubuhi.
Mwili wa Kibaki umeondolewa katika Lee Funeral Home saa 1.00 asubuhi kuelekea Othaya kwa njia ya barabara. Mazishi yatafanyika saa 10.00 jioni baada ya kupewa heshima ya mizinga 19.
Next article
Vituko vilivyoshuhudiwa wakati wa ibada ya kumuaga Kibaki