Ni kufa-kupona Utd, Atletico leo
Na MASHIRIKA
MANCHESTER United wanashuka leo ugani Old Trafford wakiwa na ulazima wa kukomoa Atletico Madrid ya Uhispania ili kufuzu kwa robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.
Ajax kutoka Uholanzi nao wataalika Benfica jijini Amsterdam wakilenga ushindi ili kutinga nane-bora. Vikosi hivyo viliambulia sare ya 2-2 katika mkondo wa kwanza nchini Ureno wiki tatu zilizopita.
Mashetani wekundu wa Man-United walilazimishia Atletico sare ya 1-1 ugani Wanda Metropolitano mnamo Februari 23.
Walifungiwa bao hilo na chipukizi Anthony Elanga aliyetokea benchi na kufuta juhudi za Joao Felix wa Atletico.
Sawa na Atletico waliopepeta Cadiz 2-1 katika mchuano wao uliopita wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Man-United nao watakuwa na ari ya kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 3-2 dhidi ya Tottenham Hotspur katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wikendi iliyopita.
Ushindi huo wa Man-United uliweka hai matumaini yao ya kukamilisha kampeni za EPL msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora na hivyo kufuzu kwa soka ya UEFA muhula ujao wa 2022-23.
Macho ya mashabiki katika gozi la leo yataelekezwa zaidi kwa nyota raia wa Ureno, Cristiano Ronaldo aliyefunga mabao yote matatu dhidi ya Spurs.
Nafuu zaidi kwa Man-United ni kwamba Ronaldo anajivunia rekodi ya kufunga mabao 25 dhidi ya Atletico hadi kufikia sasa katika mashindano yote.
Man-United walikamilisha kampeni zao za makundi kwenye UEFA msimu huu kileleni mwa Kundi F baada ya kujizolea alama 11 kutokana na mechi sita. Mabingwa hao mara 20 wa EPL walibandua Paris Saint-Germain (PSG) katika hatua ya 16-bora ya UEFA mnamo 2018-19 kwa kanuni ya bao la ugenini.
Walitoka chini baada ya kichapo cha 2-0 katika mkondo wa kwanza nchini Ufaransa na kupepeta PSG 3-1 katika marudiano ugani Old Trafford.
Hata hivyo, walishindwa kusonga mbele zaidi ya hatua ya makundi mnamo 2020-21 na hatimaye wakashuka hadi Europa League ambapo walizidiwa ujanja na Villarreal ya Uhispania.
Man-United wameshinda mechi saba kati ya 11 zilizopita katika hatua ya 16-bora ya UEFA. Hii itakuwa mara ya kwanza tangu Novemba 1991 kwa Red Devils kukutana na Atletico nchini Uingereza.
Wakati huo, vikosi hivyo viliambulia sare ya 1-1 kwenye mkondo wa pili wa mchuano wa UEFA Cup Winners’ Cup.
Ilivyo, kipute cha UEFA ndicho cha pekee kinachowapa Man-United uhalisia zaidi wa kunyanyua kombe muhula huu na kukomesha ukame wa mataji kwa miaka mitano iliyopita.
Kufikia sasa, Man-United wanashikilia nafasi ya tano kwenye jedwali la EPL kwa alama 50, moja pekee nyuma ya Arsenal ambao wana mechi tatu zaidi za kutandaza ili kufikia idadi ya michuano 29 ambayo imepigwa na vijana hao wa kocha Ralf Rangnick.
Chini ya mkufunzi Diego Simeone, Atletico sasa wameshinda mechi nne zilizopita za La Liga na wanakamata nafasi ya nne jedwalini kwa pointi 51 sawa na Barcelona.
Sawa na Man-United, kivumbi cha UEFA ndilo pambano la pekee linalowapa Atletico matumaini finyu ya kujizolea taji msimu huu.
Mabingwa hao watetezi wa La Liga walikamilisha kampeni zao za Kundi B kwenye UEFA kwa alama saba, 11 nyuma ya Liverpool ambao tayari wametinga robo-fainali baada ya kubandua Inter Milan ya Italia kwa mabao 2-1.
Ingawa Atletico walidenguliwa na Chelsea kwenye hatua ya 16-bora ya UEFA msimu jana, kikosi hicho kimetinga robo-fainali za kipute hicho mara tano kutokana na misimu minane iliyopita chini ya Simeone.
Aidha, wanajivunia rekodi ya kushinda mechi tisa kati ya 12 dhidi ya mpinzani anayeshiriki soka ya EPL katika hatua za muondoano za UEFA.
RATIBA YA UEFA (Leo)
Man-United vs Atletico (11:00pm)
Ajax vs Benfica (11:00pm)
(Kesho Jumatano)
Juventus vs Villarreal (11:00pm)Lille vs Chelsea (11:00pm)