Ni rasmi sasa 132 waliaga ajalini
Na MASHIRIKA
BEIJING, CHINA
ABIRIA 132 waliokuwa kwenye ndege ya abiria iliyoanguka kusini mwa China wiki iliyopita walifariki wote, ilisema idara ya kusimamia usafiri wa ndege nchini humo Jumamosi.
Mamia ya jamaa za waathiriwa wamekuwa wakipiga kambi kwa siku kadhaa karibu na eneo la mkasa, wakingoja ripoti kutoka kwa vikosi vya uokozi kuhusu hatima ya wapendwa wao.
Ndege hiyo ilianguka katika eneo lenye vilima vingi karibu na mji wa Wuzhou, mkoa wa Guangxi.
Ijapokuwa hakuna sababu yoyote iliyotolewa kuwa chanzo cha ajali hiyo kufikia sasa, ripoti za mwanzo zilionyesha kuwa ilianguka kutoka umbali wa futi 8,900 kwa dakika moja tu.
“Abiria wote 123 na wafanyakazi tisa wa Ndege MU5735 kutoka kampuni ya China Eastern Airlines wamethibitishwa kufariki kwenye ajali iliyofanyika Machi 21,” akasema Hu Zhenjiang, ambaye ndiye Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kusimamia Usafiri wa Ndege ya China (CAAC) kwenye kikao na wanahabari.
Akaongeza: “Tayari, miili ya abiria 120 ishatambuliwa kupitia njia ya DNA.”
Baada ya kikao hicho, washiriki wote walikimya kwa dakika moja kuwakumbuka waathiriwa wa ajali hiyo.
Maafisa wa usimamizi wa safari za ndege tayari wamethibitisha kuwa wamepata sanduku la Black Box, ambalo hurekodi masuala muhimu kuhusu ndege.
Wanasema sanduku hilo litawasaidia kubaini chanzo cha ajali hiyo baada ya kuitathmini vizuri.
Wataalamu walisema kuwa ndege hiyo aina ya Boeing 737-800 ilikuwa na visanduku viwili vya kurekodia maelezo muhimu kuihusu.
Waokozi walisema bado wanaendelea kutafuta sanduku jingine.
Usimamizi wa safari za ndege nchini humo ulitaja ajali hiyo kuwa mbaya zaidi kufanyika kwa muda wa miaka 30 iliyopita.
Next article
Karagumruk ya Shikangwa yalima Hakkarigucu inayoajiri…