Connect with us

General News

Njonjo alichangia mustakabali mwema wa taifa – Uhuru – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Njonjo alichangia mustakabali mwema wa taifa – Uhuru – Taifa Leo

Njonjo alichangia mustakabali mwema wa taifa – Uhuru

 Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta, Jumapili, Januari 2, 2022, ametangaza rasmi habari za kifo cha aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa kwanza wa asili ya Kenya, Charles Mugane Njonjo.

“Kwa huzuni mkubwa leo asubuhi, Jumapili, Januari 2, 2022, nimepokea habari za kifo cha Mheshimiwa Charles Mugane Njonjo,” akasema kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na kitengo cha habari za rais (PSCU).

Mzee Njonjo ambaye aliketi katika baraza la mawaziri la kwanza baada ya Kenya kupata uhuru mwaka 1963, alifariki saa kumi na moja alfajiri nyumbani kwake. Alikuwa na umri wa miaka 101.

Rais Kenyatta pia alimsifu marehemu hasa akitaja mchango aliotoa kwa taifa la Kenya kwa kuhudumu kama Mwanasheria Mkuu kuanzia 1963 hadi 1979.

“Kifo cha Mheshimiwa Njonjo ni pigo sio tu kwa familia yake, jamaa na marafiki bali Wakenya wote na kwa hakika bara lote la Afrika kutokana na mchango katika harakati za uhuru wa taifa la Kenya,” rais Kenyatta akasema.

Kiongozi wa taifa alisema Kenya inamshukuru Njonjo na viongozi wa kizazi chake kwa kuweka msingi wa siasa za nchi.

“Ama kwa hakika ni Mheshimiwa Njonjo na kizazi cha viongozi wa enzi ya uhuru walioweka msingi ambao taifa letu linatumia kustawi,” akasema.

Marehemu Njonjo aliingia bungeni mnamo 1980 baada ya kustaafu kama Mwanasheria Mkuu akiwa na umri wa miaka 60.

Alichaguliwa, bila kupingwa kama Mbunge wa Kikuyu, baada ya mbunge aliyekuwepo kujiuzulu siku ambapo Njonjo alitangaza nia yake ya kuwania kiti hicho.

Ni wakati huo ambapo Rais wa pili marehemu Daniel Moi alimteua Njonjo kushikilia wadhifa wa Waziri wa Masuala ya Kikatiba. Alihudumu katika cheo hicho kuanzia 1980 hadi 1983 alipopigwa kalamu kwa tuhuma za kuhusika katika jaribio la mapinduzi ya serikali mnamo Agosti 1, 1982.