ODM sasa kuchuja wanaozua vurugu
Na GEORGE ODIWUOR
CHAMA cha ODM kimebuni mbinu mpya ya kuchuja wanasiasa wanaomezea viti mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Viongozi wa chama hicho walisema kuwa wataanza kwa kuondoa wanasiasa wanaochochea vurugu.
Mwenyekiti wa ODM, Bw John Mbadi, jana alisema kuwa Baraza Kuu la chama hicho (NEC) litafungia nje wanasiasa ambao wamekuwa wakijivumisha kwa kuzua vurugu.
Ushindani mkali wa kusaka tiketi umelazimu baadhi ya wanasiasa kutumia vitisho na kuvuruga mikutano ya wapinzani wao.
Kinara wa ODM Raila Odinga amejipata njiapanda kuhusu wanasiasa watakaopewa tiketi kupeperusha bendera ya chama hicho Agosti 9, haswa katika ngome yake ya Nyanza.
Katika Kaunti ya Homa Bay, kwa mfano, Bw Mbadi, Mwakilishi wa Kike, Bi Gladys Wanga, aliyekuwa gavana wa Nairobi Evans Kidero, mbunge wa zamani wa Kasipul, Bw Oyugi Magwanga ni miongoni mwa wanasiasa ambao wametangaza azma ya kuwania ugavana kupitia tiketi ya ODM.
Katika Kaunti ya Migori, Seneta Ochillo Ayacko anamenyana na Mwakilishi wa Kike Pamela Odhiambo.Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyongo anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Seneta Fred Outa na aliyekuwa spika wa Bunge la Kaunti ya Kisumu Onyango Oloo.
Seneta wa Siaya James Orengo ambaye sasa anamezea mate ugavana, anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa aliyekuwa msemaji wa polisi, Bw Charles Owino.
Jana, Bw Mbadi alisema kuwa NEC imekuwa ikifuatilia namna wawaniaji wanaosaka tiketi ya ODM wanavyoendesha kampeni zao kwa lengo la kunasa wanaofadhili vurugu.
Mbunge huyo wa Suba alisema kuwa NEC imeagiza Bodi ya Uchaguzi ya ODM inayoongozwa na Bi Catherine Muma, kufuatilia kwa makini visa vya vurugu vinavyohusisha wanasiasa wa chama hicho wanaomezea mate viti.
Kulingana na Bw Mbadi, chama hicho kinalenga kuepuka fujo ambazo zimekuwa zikihusishwa na kura za mchujo za ODM.
“Tumegundua kuwa baadhi ya wanasiasa sasa wanatumia fujo kutishia wapinzani wao. Bodi ya uchaguzi imeagizwa kuchuja wanasiasa wa aina hiyo,” akasema Bw Mbadi akiongeza kuwa chama kinalenga kujitakasa kwa kuendesha mchujo kwa njia ya amani.“Tunatumia mbinu zote kuhakikisha kuwa kura za mchujo zinaendeshwa kwa amani,” akasema.
Wazee wa Baraza la Jamii ya Waluo katika eneo la Mbita, Suba Kaskazini, tayari wametoa wito kwa Bw Odinga kuzima wanasiasa wanaozusha vurugu wakati wa kusaka kura.
Bw Odinga mwezi uliopita alionya wanasiasa wa Nyanza dhidi ya kuzua fujo wakati wa kujivumisha. huku akisema kuwa wanafaa kuelekeza juhudi zao katika kiti cha urais.
Kinara huyo wa Azimio la Umoja, alisema vurugu hizo huenda zikatatiza juhudi zake za kutaka kumrithi Rais Uhuru Kenyatta baada ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Next article
Keki ya Raila kukatwa katika kaunti zote 47