ODM yakwepa mchujo kaunti ishirini na sita
NA LEONARD ONYANGO
CHAMA cha ODM hakitafanya kura za mchujo katika Kaunti 26 – ishara kwamba huenda kikawapa tiketi za moja kwa moja wawaniaji wa maeneo hayo au kuachia vyama vilivyo ndani ya muungano wa Azimio la Umoja.
Kulingana na mwenyekiti wa Bodi ya Uchaguzi (NEB) ya ODM Catherine Mumma, kura za mchujo zitafanyika katika kaunti 21 kati ya Aprili 1 na Aprili 21.
Kura za mchujo zitafanyika katika Kaunti za Nakuru na Turkana Ijumaa ijayo.
“Kura za mchujo zitafanyika katika vituo ambavyo wawaniaji wataelewana,” akasema Bi Mumma.
Katika Kaunti za Narok na Kajiado, kura za mchujo zitafanyika Jumamosi ijayo, kwa mujibu wa ratiba ya ODM.
Kura za mchujo katika kaunti za Kilifi na Tana River zitafanyika Aprili 4 na siku itakayofuatia shughuli hiyo itahamia katika kaunti jirani za Taita Taveta na Kwale.
Kinyang’anyiro kigumu kinatarajiwa katika Kaunti ya Mombasa Aprili 6 ambapo mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir na mfanyabiashara Shahbal Suleiman watakuwa wanamenyana kusaka tiketi ya ugavana.
Katika Kaunti za Kisii na Nyamira, kura hizo zitafanyika Aprili 7 na Vihiga na Busia zitafanyika Aprili 12.
Ushindani mkali unatarajiwa katika Kaunti za Kisumu na Siaya Aprili 13 na Siaya Aprili 14 mtawalia.
Kaunti hizo ndizo ngome ya kinara wa ODM Raila Odinga na watakaofanikiwa kupata tiketi watakuwa na nafasi bora ya kuchaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.
Katika Kaunti za Bungoma, kura za mchujo zitafanyka katika Kaunti za Bungoma na Trans-Nzoia Aprili 15 na kisha shughuli hiyo kuelekea katika Kaunti ya Migori Aprili 16 ambayo pia ni ngome ya Bw Odinga.
Mwenyekiti wa ODM John Mbadi na Mwakilishi wa Wanawake Bi Gladys Wanga – ambao wote wanawania ugavana wa Homa Bay kupitia tiketi ya ODM watajua hatima yao Aprili 18.
Shughuli ya kura za mchujo itakamilishwa katika kaunti za Kakamega (Aprili 19) na Nairobi Aprili 21.
Kulingana na Bi Mumma, ni wanachama wa ODM tu watakaoshiriki kura za mchujo. Kura za mchujo za ODM zimekuwa zikikumbwa na vurugu na visa vya udanganyifu.
Chama hicho cha Bw Odinga kinaonekana kukwepa kaunti za maeneo ya Mlima Kenya, Kaskazini Mashariki na Bonde la Ufa.
Watakaoshinda tiketi ya ODM pia huenda wakalazimika kuachia wenzao wa vyama vilivyo ndani ya muungano wa Azimio la Umoja kutokana na hofu ya kugawanya kura na kutoa fursa kwa chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Naibu wa Rais William Ruto kupata ushindi.
Chama cha UDA kimetangaza kuwa kitafanya kura za mchujo kote nchini Aprili 14.
Wanasiasa watakaobwagwa kwenye kura za mchujo watakuwa na fursa ya kugombea kama wawaniaji huru katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Chama cha Jubilee ambacho ni mshirika wa Azimio la Umoja, kimekuwa kikishinikiza ODM kutosimamisha wawaniaji katika eneo la Mlima Kenya, Nakuru, Kajiado, Narok na Nairobi.
Chama tawala kimesisitiza kuwa kinalenga kupata idadi kubwa ya wabunge watakaosaidia Rais Uhuru Kenyatta kudhibiti serikali ya Bw Odinga iwapo atachaguliwa kuwa rais kwenye Uchaguzi mkuu ujao.
Vyama vidogo zaidi ya 20 vilivyomo ndani ya Azimio pia vimekuwa vikishinikiza ODM kutosimamisha katika maeneo ambapo vina ushawishi.
Chama cha Democratic Action Party-Kenya (DAP-K) kinachoongozwa na Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa, pia kimeshikilia kuwa kitamenyana na ODM katika maeneo yote nchini.