ODM yaonya wanasiasa wake dhidi ya kuzua vurugu
NA MAUREEN ONGALA
BODI ya Kitaifa ya Uchaguzi katika chama cha ODM, imeonya wanasiasa kuwa watapigwa marufuku kushiriki katika uchaguzi ujao iwapo watachochea vurugu.
Hii ni baada ya rabsha kutokea wakati wa mkutano wa wagombeaji watarajiwa wa ODM katika Kaunti ya Kilifi.
Kamishna wa bodi hiyo, Bw Elisha Thairo alisema mtu yeyote atakayethibitishwa kuchochea ghasia hatakubaliwa kuwania tikiti ya chama kuelekea katika uchaguzi mkuu ujao.
“Hatutavumilia fujo za aina yoyote kutoka kwa wanasiasa katika kipindi cha uchaguzi. Iwapo tutabaini kwamba wewe au wafuasi wako ndio wanasababisha ghasia, tutakupiga marufuku kushiriki uchaguzi,” akasema.
Katika mkutano ulioandaliwa Ijumaa mjini Kilifi, wafuasi wa wanasiasa wanaotaka kuwania ugavana walizozana na kutatiza mkutano huo kwa dakika kadhaa hadi wakatulizwa.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria ni wale wanaotaka kuwania tikiti za ODM kwa ugavana, akiwemo waziri msaidizi wa Ugatuzi aliyejiuzulu, Bw Gideon Mung’aro, Naibu Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Saburi, na Spika wa Bunge la Kaunti ya Kilifi, Bw Jimmy Kahindi.
Huku akihakikishia wanachama kwamba kura ya mchujo itafanywa kwa njia ya haki, alisema ratiba kuhusu shughuli hiyo imepangwa kutolewa rasmi wiki hii.
“Sisi sote ni wanachama wa ODM na hatutaki kumkosesha yeyote haki kwa sababu ni kupitia kwa haki pekee ambapo tutakuwa na nguvu zaidi,” akasema.
Mwenyekiti wa ODM, tawi la Kilifi, Bw Teddy Mwambire aliomba wanasiasa waeke kando tofauti zao na kutaka maafisa wa chama kuruhusu kila mwa – niaji tikiti aendeshe kampeni zake bila ubaguzi.
“Waratibu wa chama mashinani na katika maeneobunge, lazima muwakaribishe wagombeaji wote kufanya mikutano ha hadhara na kuhutubia wanachama na pia kuendesha kampeni bila vikwazo,” akasema.
Next article
Wazee wafanya Rais ajikune kichwa zaidi