Omanga amtetea Ruto kwa kuahidi kuwapiga jeki makahaba
Na CHARLES WASONGA
SENETA Maalum Millicent Omanga ndiye mwandani wa kwanza wa Naibu Rais William Ruto kujitokeza waziwazi kumtetea kuhusiana na kauli aliyotoa kuhusu makahaba akiwa Mtito Andei, Jumatatu.
Akiwa katika ziara za kusaka uungwaji mkono kushinda urais 2022 katika Kaunti ya Makueni, Dkt Ruto aliwashauri wanawake wanaoshiriki biashara hiyo kubuni Shirika la Akiba na Mikopo (SACCO) la kuwasaidia kuwekeza katika biashara halali.
Dkt Ruto aliahidi kuweka Sh1 milioni katika shirika hilo ili kama hatua ya kuwasaidia wanawake hao kufikia lengo hilo.
“Pesa hizi zitawasaidia ninyi kuanzisha biashara ya heshima badala ya kuuza miili yenu huku na kule ili kujisaidia,” Dkt Ruto akasema.
Naibu Rais alitoa ahadi hiyo baada ya mwanamke mmoja kujitambulisha kama kahaba mjini Mtito Andei, na kumuomba msaada akisema ameathirika zaidi kiuchumi kutokana na janga la Covid-19.
Kauli hiyo ilikosolewa na Wakenya mitandaoni huku wengine wao wakidai kuwa “anaendeleza biashara hiyo haramu iliyopigwa marufuku.”
Wengine walihoji aina ya serikali ambayo Dkt Ruto anapania kuazisha endapo atashinda katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Lakini Ijumaa Seneta Omanga alijitokeza kimasomaso kumtetea ‘bosi’ wake akisema kuwa ahadi ya Dkt Ruto ililenga kuwaondoa makahaba wa Mtito Andei kutoka biashara hiyo haramu na wala hakulenga kuiendeleza.
“Naibu Rais alilenga kuwasaidia wanawake hao kuanzisha biashara nzuri na za heshima zitakazowasaidia badala ya kuuza miili yao. Nimefurahi kwamba tangazo hili lililotolewa Kibwezi limeibua mjadala kitaifa,” Bi Omanga akasema kupitia ujumbe katika akaunti yake ya Twitter.
Lakini Silvester Nyaberi akasema kupitia Facebook: “Ni wapi katika kanisa au katika Bibilia ambapo ukahaba unaruhusiwa? Ruto anaongozwa na uchu wa urais kiasi kwamba anaahidi kila kitu ili apate kura.”
Naye Saul Ouma akasema: “Sacco haitawasaidia kwa sababu watahitaji kufanya kazi kuijenga. Kwa sababu bado watahitaji fedha, watalazimika kurejelea ukahaba.”
Nchini Kenya ni kinyume cha sheria kwa mtu yeyote kufaidi kutokana na ukahaba, kusaidia, kuiendeleza, kulazimisha au kuchochea biashara ya ngono.