Omanyala, Kemboi kutimka katika mbio za kuinua sifa ya Kenya kwenye maonyesho ya Dubai
Na MICHAEL KIRWA
MSHIKILIZI wa rekodi ya Afrika mbio za mita 100, Ferdinand Omanyala na Wakenya wengine sita walielekea nchini Milki za Kiarabu mnamo Jumatano usiku kushiriki mbio za 2021 Dubai Run.
Mbio hizo zinazofahamika kama “Run with the Champions”, zitashuhudia washiriki akiwemo Mwana wa Mfalme wa mji wa Dubai, Sheikh Hamdan bin Mohammed, akitimka mbio za kilomita tano na 10 katika barabara kuu ya Sheikh Zayed mnamo Novemba 26.
Mbio za 2021 Dubai Run ni baadhi ya shughuli kadhaa zilizo kwenye menyu ya wanariadha hao saba kutoka Kenya katika maonyesho ya Dubai 2020.
Shirika la Kukuza Usafirishaji Bidhaa na Chapa la Kenya (KEPROBA), ambalo litaendesha kibanda cha Kenya katika maonyesho hayo, linalenga kunadi Kenya kama eneo muhimu la uwekezaji, michezo na utalii.
Mbali na Omanyala, ambaye aliweka rekodi ya kitaifa na Afrika ya mbio za mita 100 ya sekunde 9.77 kwenye mashindano ya Kip Keino Classic ugani Kasarani mwezi Septemba, pia kuna bingwa mara mbili za Olimpiki mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Ezekiel Kemboi.
Vilevile, kuna bingwa wa zamani wa dunia mbio za mita 800 Janeth Jepkosgei, mshindi wa London Marathon mwaka 2013 Priscah Jeptoo, Bethwel Yegon aliyekamata nambari mbili mbio za Berlin Marathon 2021, Jonathan Kiplimo Maiyo anayejivunia muda wake bora kwenye marathon wa saa 2:04:56 kutoka Dubai Marathon 2012 na mshindi wa Nagpur Half Marathon mwaka 2010 Hellen Nzembi.
Omanyala atakuwa kiongozi wa timu hiyo ya wanariadha kutoka Kenya. Atatimka mbio za kilomita tatu katika maonyesho hayo.
“Ni heshima kubwa kuungana na magwiji kama Ezekiel Kemboi na Janeth Jepkosgei kunadi taifa letu kupitia mradi wa kufurahia na kuvutia kama huu. Mbali na kuonyesha talanta bora ya taifa langu, pia natumai kujifunza kutoka kwa mataifa mengine,” aliongeza.
Omanyala yuko mapumzikoni wakati huu kabla ya kuanza msimu wenye shughuli nyingi kuanzia Februari mwaka 2022.
Baadhi ya mashindano anayotarajiwa kushiriki ni pamoja na Riadha za Dunia za Ukumbini, Kip Keino Classic, Diamond League, Continental Tour, Riadha za Bara Afrika, Riadha za Dunia na Michezo ya Jumuiya ya Madola.
Mashindano hayo yote yatafanyika ndani ya kipindi cha miezi sita.
Mjini Dubai, mbio zitaanzia katika hema la Kenya na zitajumuisha kilomita tatu, tano na 10.
Jepkosgei alisema anasubiri kwa hamu kubwa kuonyesha talanta ya hali ya juu kutoka Kenya katika sekta ya kilimo na utalii.
“Nasubiri kwa hamu kubwa kufanya majukumu yangu katika maonyesho hayo. Nitaeleza dunia kuhusu taifa letu ambalo ni la amani na karimu, bidhaa zetu za hali ya juu za kilimo, na maeneo ya kuvutia ya kitalii,” alisema Jepkosgei, 37, ambaye sasa ni kocha.
Maonyesho haya ya Dubai 2020 yaliratibiwa kuandaliwa kutoka Oktoba 20, 2020 hadi Aprili 10, 2021, lakini yakafutiliwa mbali kutokana na hofu ya maambukizi ya virusi vya corona.
“Wanariadha ni mabalozi wetu wakubwa. Wao kuwa katika kibanda cha Kenya watainua juhudi zetu za kunadi Kenya kama eneo muhimu la uwekezaji, michezo na utalii,” alisema Afisa Mkuu Mtendaji wa Keproba, Wilfred Marube wakati wa kuwapa wanariadha hao bendera ya Kenya jijini Nairobi mnamo Jumatano.
TAFSIRI: GEOFFREY ANENE