Patrick ‘Jungle’ Wainaina kuwania ugavana kwa tiketi ya kujitegemea
NA LAWRENCE ONGARO
MBUNGE wa Thika, Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, amesema atawania kiti cha ugavana katika kaunti ya Kiambu akitumia tikiti ya kujitegemea (Independent).
Alifikia uamuzi huo baada ya kushindwa na seneta wa Kiambu Kimani Wamatangi kwenye mchujo wa kuwania tikiti ya UDA.
Akihutubia waandishi wa habari, Bw Wainaina alisema makarani wa kusimamia uchaguzi huo walimpendelea Bw Wamatangi.
“Maafisa hao walikosa kuangazia jina langu la ‘Wajungle’ ambalo linajulikana na wengi. Tena wafuasi wangu walichanganyikiwa baada ya kukosa jina hilo kwenye orodha ya majina mengine,” alisema mbunge huyo.
Alidai kuwa uchaguzi huo haukuwa wa haki na uwazi kwa sababu maajenti wake walifurushwa nje wakati wa kuhesabu kura hizo.
“Ningetaka kuwahakikishia wafuasi wangu waendelee kuvuta subira kwani bado ninapanga mikakati kuona ya kwamba ninashiriki katika uchaguzi mkuu ujao wa Agosti 9, 2022,” alifafanua mbunge huyo.
Alieleza kuwa hivi karibuni ataanza kuzuru maeneo mengi ya Kiambu ili kuvumisha kampeni zake katika kaunti nzima ya Kiambu.
” Nina imani na wapigakura wa Kiambu kuwa wataniunga mkono kwa kunichagua niwe gavana wao ifikapo wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022,” alisema Bw Wainaina.
“Sina imani na matokeo hayo kwa sababu mpinzani wangu, Wamatangi, alipiga kambi katika Chuo cha Kiufundi na Teknolojia cha Kiambu Institute of Science and Technology akiandamana na wafuasi wake. Pia alijuana vyema na maafisa wa kuhesabu kura,” akaongeza kusema mbunge huyo.
Mwingine aliyedai kuibiwa kura zake ni seneta maalum Bw Isaac Mwaura aliyetaka tiketi ya kuwania kiti cha ubunge Ruiru. Alidai kwamba kura zake ziliibiwa akipambana na mbunge wa Ruiru, Bw Simon King’ara.
Hata hivyo amesema atashirikiana na mwenzake Simon King’ara ili kuleta amani kwa chama cha UDA.
Alikitaka chama cha UDA kuchukua jukumu kuona ya kwamba mambo yanarekebishwa haraka iwezekanavyo ama wafuasi wengi wakihame.
Baadhi ya viongozi waliopata tikiti ya UDA, ni Kigo Njenga wa Gatundu Kaskazini na George Koimburi ambaye ni mbunge wa Juja.
Wengine wanaogombea kiti cha ugavana na tikiti tofauti ni gavana wa sasa wa Kiambu Dkt James Nyoro (Jubilee), Moses Kuria wa Chama Cha kazi (CCK), na Bw William Kabogo wa Tujibebe Party.