Pigo kwa Ruto Musalia akinasa mwandani wake
DERICK LUVEGA na VICTOR RABALLA
NAIBU Rais William Ruto anaendelea kupata pigo katika juhudi zake za kuimarisha uungwaji mkono maeneo ya Magharibi na Nyanza baada ya wandani wake wakuu kugura kambi yake.
Siku chache baada ya kumpoteza mshirika wake mkuu katika Kaunti ya Kisii, Naibu Gavana Joash Maangi, mwandani wake mwingine, Mbunge wa Hamisi, Bw Charles Gimose, amemtoroka.
Bw Gimose amejiunga na chama cha Amani National Congress (ANC) kinachoongozwa na Bw Musalia Mudavadi.
Agura Tangatanga
Mbunge huyo aligura kambi ya Tangatanga baada ya Dkt Ruto kufanya ziara ya siku mbili katika Kaunti yake ya Vihiga.
Kwa upande wake Gavana wa Migori Okoth Obado, amekana kuunga mkono azma ya Naibu Rais ya kuingia Ikulu 2022 akisema wakati huu anajishughulisha na uvumishaji wa chama chake cha People Development Party (PDP).
Akitangaza kuhama kwake kutoka kambi ya Tangatanga, Bw Gimose alisema hivi: “Nilikuwa nimeenda tu kuwalisha mifugo. Nimerejea nyumbani. Ng’ombe wakipelekwa malishoni, hurejea nyumbani.”
Bw Gimose alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha Ford Kenya kinachoongozwa na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula. Baada ya uchaguzi mkuu wa 2017 , mbunge huyo alianza kufanyakazi na Dkt Ruto.
Ni kupitia mbunge huyo ambapo Naibu Rais aliweza kupenya kaunti ya Vihiga na kufaulu kufanya mikutano kadha ya kisiasa katika eneo bunge la Hamisi ambalo lilionekana kwenda kinyume na mawimbi ya siasa za ANC.
Hatua ya Bw Gimose kuhamia kambi ya ANC, sasa imeimarisha ushawishi wa Bw Mudavadi katika Kaunti ya Vihiga.
Ushawishi wa Mudavadi
Hiyo ina maana kuwa sita kati ya wabunge saba katika kaunti wako upande wake, kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022. Ni mbunge wa Luanda Chris Omulele pekee ambaye amesalia mshirika wa kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Bw Gimose alisema amekuwa akifuatilia hali ya kisiasa katika Kaunti ya Vihiga na kote nchini tangu wakati wa mazishi ya mamake Mudavadi, marehemu Hanna Atsianzale Mudavadi.
Katika Kaunti ya Kisii, Bw Maangi aliwaacha wakazi vinywa wazi alipohudhuria mkutano wa Azimio la Umoja katika uwanja wa Kasarani, Nairobi mnamo Desemba 10.
Bw Maangi ambaye amekuwa mshirika mkuu wa Dkt Ruto katika eneo zima la Gusii, alitangaza kuwa amerejea ODM na kwamba anaunga mkono azma ya Bw Odinga. Bw Maangi pia ameahidi kumshawishi Gavana Obado arejee ODM.
“Jinsi mjuavyo, tumekuwa upande ule mwingine na Gavana Obado. Nitaongea naye kisha nimpeleke kwa Profesa Anyang’ Nyong’o (Gavana wa Kisumu) ili sote twende kwa Bw Odinga,” alisema mwishoni mwa juma lililopita akiwa mjini Kisumu.
Aliongeza, “Kama viongozi wa Nyanza, tunafaa kuungana chini ya uongozi wa kiongozi wa chama chetu ili afaulu kuwa Rais wa tano wa Kenya.”
Next article
TUSIJE TUKASAHAU: Undumakuwili wa Ruto kuhusu hatimiliki…