Pigo kwa uchumi pato la kilimo likishuka mno
LEONARD ONYANGO na CECIL ODONGO
RIPOTI ya Kuhusu Hali ya Uchumi wa Nchi 2022 Alhamisi ilifichua kuwa sekta ya Kilimo iliathirika zaidi mwaka 2021 kimapato ikilinganishwa na 2020.
Kiwango cha mapato kilipungua kutoka asilimia 5.2 hadi asilimia tano.
Ukosefu wa mvua ulichangia kupungua kwa mavuno katika sekta ya majanichai, mahindi na ngano.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kiwango cha mahindi kilichozalishwa kilipungua hadi magunia milioni 36.7 kutoka magunia milioni 42.1 mnamo 2020.
Kahawa iliyozalishwa nayo ilipungua kwa asilimia sita hadi tani 34,500 nayo majani chai ilipungua kwa asilimia 5.6 hadi tani 537, 800.
“Hali hii ilichangiwa na hali ya anga isiyotabirika katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa ujumla kiwango cha uzalishaji kilipungua katika mimea na ufugaji,” ikasema ripoti hiyo.
Aidha thamani ya mahindi yaliyouzwa ilipungua kutoka Sh8.2 bilioni hadi Sh6.9 bilioni kati ya 2020 na mwaka uliopita kutokana na kupungua kwa kiwango cha uzalishaji.
Ingawa kiwango cha majanichai na kahawa kilichozalishwa kilipungua, thamani yao ilipanda sokoni kutoka Sh18.6 milioni hadi Sh10.8 milioni mnamo 2021.
Mapato yanayotokana na majanichai pia yalipanda licha ya uzalishaji wa chini kwa asilimia 3.2 hadi Sh126 bilioni.
“Uzalishaji wa kahawa ulipungua kutokana na gharama ya juu ya pembejeo za kilimo pamoja na uvamizi wa wadudu. Pia hali ya anga isiyoridhisha ilichangia kupungua kwa uzalishaji wake,” ikaongeza ripoti hiyo.
Hata hivyo, kiwango cha uzalishaji nacho kilipanda katika sekta ya kilimo cha miwa kutoka tani milioni 6.8 hadi milioni 7.8 mnamo 2021.
Bidhaa nyingine za kilimo ambazo bei zao sokoni zilipanda ni maziwa ambayo yaliuzwa kwa Sh33.7 bilioni na kilimo cha maua ambacho kililetea nchi Sh157.7 bilioni.
Licha ya kupungua kwa uzalishaji, sekta ya Kilimo bado ilitekeleza jukumu muhimu katika kuimarisha uchumi wa Kenya kwa kuwa ilichangia asilimia 22.4 ya mapato ya nchi.
Idara nyingine za uchukuzi, ujenzi wa makazi, biashara na miradi mingine zilichangia asilimia 11.4, 8.9, 7.9 na huduma nyingine mtawalia. Ushuru ambao huchangia pakubwa katika kuendesha uchumi, ulichangia asilimia 8.2 katika mapato yote ya chini mnamo 2021.
Mfumko wa kiuchumi nchini nao ulipanda hadi asilimia 6.1 ambayo ni kiwango cha juu zaidi kutokea tangu mnamo 2018.
Mnamo 2020, mfumuko wa kiuchumi ulikuwa asilimia 5.4.
Reli ya Kisasa (SGR) ilizalisha pato la Sh15.2 bilioni mwaka 2021, hilo likiashiria kuwa mradi huo haujafikia malengo ya kimapato yaliyowekwa tangu uzinduzi wake miaka mitano iliyopita.
Kiwango hicho ni asilimia 12.6 zaidi ya pato lililozalishwa mnamo 2020. Reli hiyo ilizalisha pato la Sh13.5 bilioni mwaka huo.
Kulingana ripoti hiyo, huduma za uchukuzi wa mizigo zilileta mapato ya Sh13 bilioni, huku ubebaji abiria ukileta faida ya Sh2.2 bilioni.
Kiwango hicho hakitoshi kugharimia uendeshaji wa mradi huo, unaokisiwa kutumia Sh1.5 bilioni kila mwezi.
Hilo linamaanisha matumizi yake hugharimu jumla ya Sh18 bilioni kwa mwaka.
Garimoshi huwa linawabeba abiria kutoka jijini Nairobi hadi Mombasa; likiwa na steji katika maeneo ya Athi River, Emali, Kibwezi, Mtito Andei, Voi, Miasenyi na Mariakani.
Mnamo 2018, ripoti kutoka Shirika la Kukusanya Takwimu Kenya (KNBS) ilionyesha kuwa reli hiyo ilizalisha pato la Sh5.5 bilioni.
Aidha ripoti hiyo pia ilionyesha kuwa karibu Wakenya 926,000 walipata ajira mwaka uliopita wakati ambapo uchumi nao ulikua na kufika asilimia 7.5.
Next article
AS Roma yazamisha Leicester City na kutinga fainali ya…