Polisi wapeleleza biashara chafu ya filamu za ngono
Na BRIAN OCHARO
WAPELEZI jijini Mombasa wameanzisha uchunguzi wa biashara haramu ya filamu za ngono kimataifa.
Inashukiwa mitandao ya nchi za kigeni hushirikiana na wafanyikazi wa nyumbani kurekodi filamu hizo bila wazazi kujua, na kuzisambaza kupitia kwa intaneti.
Majasusi walisema wameanzisha uchunguzi huo baada ya kukamata mwanamke ambaye alikubali mahakamani kwamba alimnajisi mvulana wa miaka minne.
Polisi walidai kuwa alirekodi kitendo hicho kwa simu na inashukiwa alinuia kutumia video hiyo kwa biashara haramu ya uuzaji wa filamu za ngono mitandaoni.
Mwanamke huyo amewekwa kizuizini kuwasaidia wapelelezi kutoka Kitengo cha Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu na kile cha Ulinzi wa Watoto ili kubaini kama kuna washirika wake humu nchini.
Bw Andrew Warui, anayeongoza kitengo hicho eneo la Pwani, alisema wapelelezi walimkamata mwanamke huyo baada ya kufanya uchunguzi kwa miezi mitatu.
Kulingana naye, kuna visa kadhaa vingine vinavyochunguzwa ambapo watoto walio na umri wa kuanzia miaka minne wamenajisiwa na walezi wao na kanda za vitendo hivyo haramu kusambazwa kupitia mitandao mbalimbali.
“Tunafuatilia visa kama hivyo katika Kaunti za Kilifi na Mombasa. Pia tunajaribu kukatiza usambazaji wa kanda hizo za unyanyasaji wa watoto mtandaoni,” akasema.
Mwanamke aliyekamatwa, alifikishwa katika Mahakama ya Shanzu na kukiri kosa la kumnyanyasa kingono mvulana katika makazi yao mtaa wa Kisauni.
Mahakama iliambiwa kuwa mshukiwa alitenda makosa hayo kati ya Juni 2020 na Oktoba 2021.
Hata hivyo, alikanusha shtaka la kurekodi filamu hiyo alipofika mbele ya Hakimu Mkuu Florence Macharia.
Mahakama iliambiwa kuwa mwanamke huyo, ambaye aliajiriwa na wazazi wa mtoto husika, aliacha kazi Oktoba mwaka jana.
Siku chache baada ya kuacha kazi, mama wa mtoto alipokea video hiyo kutoka kwa nambari ya kigeni kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp.
“Baada ya kuufungua ujumbe huo, mama aliona video ya mshukiwa na mtoto. Alikuwa akimnyanyasa mvulana huyo kingono,” mwendesha mashtaka alisema.
Baada ya kutazama video hiyo, mama wa mtoto huyo alijaribu kumtafuta mshukiwa huyo lakini hakuweza kupatikana kwa nambari zake za simu za mkononi zilikuwa zimezimwa.
Mama huyo alimuonyesha mumewe video hiyo kisha wakaripoti kwa polisi.
Uchunguzi ulianza na baada ya siku chache alikamatwa na simu aliyokuwa akitumia ikatwaliwa.
Uchunguzi wa simu hiyo ulionyesha mshukiwa alituma ujumbe kwa wazazi wa mtoto huyo akitaka alipwe fedha.
Polisi walidai kuwa uchambuzi wa simu hiyo ulionyesha mshukiwa alituma video hiyo kwa nambari kadhaa za kigeni na kupokea malipo.
Mwanamke huyo alidai kuwa alilazimishwa kufanya kitendo hicho na rafiki aliyejulikana tu kama Joshua ambaye alikutana naye kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook ambaye alimuahidi kazi ya duka kubwa.
Next article
Maafisa wa kaunti wajiandaa kujiuzulu ili kuingia kwa siasa