WANDERI KAMAU: Polisi wasiwabague wale walio na digrii wanapoajiri maafisa wapya
NA WANDERI KAMAU
HATUA ya Huduma ya Kitaifa ya Kuwaajiri Polisi (NPSC) kutangaza haitakuwa ikiwaajiri mahafala kutoka vyuo vikuu ni pigo kubwa kwa juhudi za kutatua shida ya ukosefu wa ajira nchini miongoni mwa vijana.
Katika kutoa tangazo hilo, idara hiyo ilisema mahafala wamegeuka kuwa “wasumbufu” baada yao kuishtaki kwa tuhuma za kupunguza mishahara yao katika hali tatanishi mwaka uliopita.Idara sasa inasema itakuwa ikiwaajiri vijana waliofikisha alama ya D+ kwenda chini “kwani ndicho kiwango kinachohitajika.”
Tangazo hilo ni pigo kwa maelfu ya vijana ambao wanamaliza masomo yao katika taasisi za elimu ya juu na kuanza kuhangaika kutokana na ukosefu wa kazi.
Mwelekeo huo pia unaashiria kwamba idara hiyo inashabikia kuwepo kwa makurutu wa elimu ya kiwango cha chini, licha ya mabadiliko makubwa kwenye mazingira ya utendakazi katika siku za hivi karibuni.
Kwa sasa, polisi wanahitaji ujuzi wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) ili kukabiliana vilivyo na wahalifu.
Ikumbukwe kuwa, wahalifu wamebadilisha mbinu zao wa uhalifu, ambapo kinyume na zamani, wengi wanatumia mitambo ya kisasa kuendesha visa vya uhalifu.
Kwa mfano, wezi wa benki hawatumii bunduki kama ilivyokuwa miaka ya sabini na themanini, bali wanatumia ujuzi wa ICT kuingilia mitambo ya taasisi za kifedha wanakolenga kutekeleza uhalifu.
Katika hali hiyo, ni dhahiri kwamba ni hatua isiyofaa kwa polisi kuonekana kushabikia uwepo wa watu ambao hawana ufahamu wa masuala kama hayo kwa kufutilia mbali uajiri wa mahafala.
Maswali yanayoibuka ni: idara hii imejitayarisha kukabiliana na mabadiliko ya mbinu za uhalifu? Ni hatua inayolenga kuwapa mwanya wahalifu kuendeleza juhudi zao kuwahangaisha wananchi?
Kwa muda mrefu, idara ya polisi ilihusishwa na visa vya ukatili.
Idara haikuonekana kuwa na uso wa kumjali mwananchi, bali ilionekana kama adui wa raia.
Hata hivyo, juhudi za kubadilisha dhana hiyo zilianza baada ya kupitishwa kwa Katiba Mpya ya 2010.
Kinachosikitisha ni kuwa, licha ya hatua zote ambazo zimepigwa kuigeuza idara hiyo ili kuifanya kuwa taasisi ya kisasa, hilo linairejesha katika enzi ya giza.
Wito wetu kwa serikali ni kutathmini upya uamuzi huo ili kuwapa matumaini maelfu ya vijana waliosoma na bado wanahangaika kutafuta kazi.
[email protected]