Polisi watano wapinga tuhuma katika kesi ambapo mahabusu alifariki ndani ya seli
Na RICHARD MUNGUTI
MAAFISA watano wa polisi wanaopinga kushtakiwa kwa mauaji ya mahabusu ndani ya seli wanaomba mahakama kuu isitishe kesi inayowakabili na badala yake iamuru uchunguzi wa kubaini kilichosababisha kifo cha Caleb Otieno Espino mwaka 2018.
Otieno alifia katika seli ya Kituo cha Polisi cha Changamwe kaunti ya Mombasa mnamo Septemba 17, 2018.
Maafisa hao Khalif Abdullahi Sigat, James Muli Koti, Joseph Odhiambo Sirawa, Edwarde Kongo Onchonga na Nelson Nkanae wanadai kushtakiwa kosa la kutekeleza mauaji kumekiuka haki zao kwa mujibu wa Sheria za Uhalifu nambari 386 na 387 na pia Kifungu nambari 157 (11) cha Katiba.
Kwa mujibu wa sheria hizo tatu, imeagizwa mshukiwa akifa akiwa mikononi mwa polisi ama idara ya magereza hakimu aliyekaribu na mahala pa maafa anatakiwa kufanya uchunguzi kutathmini kilichosababisha kifo hicho.
Katika kisa cha Otieno, aliyeaga dunia akiwa katika kituo cha polisi cha Changamwe, polisi hao wanasema hakimu mkuu wa mahakama ya Mombasa angefanya uchunguzi kubaini kilichosababisha kifo cha mahabusu huyo.
Polisi hao wanaomba mahakama ibatilishe uamuzi wa hapo awali.
Watano hao walishtakiwa Septemba 13, 2021 katika Mahakama kuu ya Nairobi kwa kosa la kutekeleza mauaji.
Watano hao walikanusha mashtaka dhidi yao mbele ya Jaji Justus Momanyi Bwonwong’a.
Ombi lao la kuachiliwa kwa dhama ilikataliwa na Jaji Bwonwong’a.
Jaji Bwonwong’a aliorodhesha kesi hiyo kusikilizwa lakini Bw Omari akawasilisha ombi la kuisitisha hadi ombi alilowasilisha lisikilizwe na kuamuliwa.
Katika kesi hiyo, watano hao wanaomba uamuzi wa kuwafungulia shtaka la kutekeleza mauaji ubatilishwe kisha agizo la uchunguzi kubaini kilichosababisha kifo cha Otieno ndani ya seli.
Washtakiwa hao wanaiomba korti ifutilie mbali shtaka hilo la mauaji na kuagiza uchunguzi wa kubaini kifo cha Otieno ufanywe mara moja.
“Endapo hii mahakama haitaamua ombi hili kwa upesi, haki za washtakiwa zitakandamizwa ikitiliwa maanani mhasiriwa alifariki katika mazingira tata,” polisi hao warai.
Uchunguzi wa kifo cha Otieno ulifanywa na mamlaka huru ya polisi (IPOA) kisha wakapendekezea mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) Noordin Haji awashtaki polisi hao kwa mauaji.
Polisi hao wameeleza endapo korti haitaingilia kati na kuwaachilia kwa dhamana, basi DPP ataendelea kuvuruga haki zao.
Pia wanaomba korti iamuru afisa anayechunguza kesi hiyo John Maranya ahonjiwe sababu za kukataa washtakiwa wakiachiliwa kwa dhamana.
Uamuzi wa kuwashtaki watano hao wa mauaji, Jaji Bwonwong’a alifahamishwa ni ukiukaji wa sheria.
Kiongozi wa mashtaka Solomon Naulikha aliomba muda kujibu tetezi hizo za washtakiwa hao.
Aliomba muda wa wiki mbili.
Next article
Benitez katika presha ya kupigwa kalamu baada ya Everton…