Connect with us

General News

Putin asababishia Wakenya kero kuu – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Putin asababishia Wakenya kero kuu – Taifa Leo

Putin asababishia Wakenya kero kuu

NA CHARLES WASONGA

RAIS Vladimir Putin wa Urusi amevuruga uchumi wa Wakenya kwa kushambulia jirani yake Ukraine siku 14 zilizopita.

Tayari bei za bidhaa za kimsingi kama vile gesi ya kupikia imepanda kutokana na vita hivyo, licha ya Kenya kuwa umbali wa takriban kilomita 9,000 kutoka vita hivyo vinakoendelea.

Athari za vita hivyo zimefika Kenya kutokana na kuwa Urusi na Ukraine ni washirika wakuu kibiashara wa Kenya hasa bidhaa za kilimo, mbolea, gesi ya kupikia, mafuta na mabati yanayotumika katika sekta ya ujenzi.

Vita kati ya mataifa hayo mawili pia vimevuruga soko la mazao ya kilimo kama vile majani chai na parachichi ambayo Kenya huuza kwa wingi katika mataifa hayo ya Uropa Mashariki.

Bei ya mafuta inatarajiwa kupanda wiki ijayo kufuatia ongezeko la bei ya bidhaa hiyo kimataifa kutokana na vita hivyo, na vikwazo ambavyo Amerika na mataifa washirika wake yameiwekea Urusi.

Mnamo Jumatatu, bei ya pipa moja la mafuta ghafi ilipanda hadi Sh14,000, ongezeko la juu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 14.

Urusi ni taifa la tatu duniani katika uzalishaji wa mafuta, lakini vita hivyo na vikwazo ilivyowekewa vimeathiri uwezo wake wa kuuza bidhaa hiyo ng’ambo.

Hii ina maana kuwa kuna uwekezano mkubwa kwamba bei ya mafuta itapanda wiki ijayo ikilinganishwa nay a sasa ya Sh129 (petroli), Sh110 (dizeli) na Sh105 (mafuta taa), hatua ambayo itaongeza gharama ya maisha kwani mafuta hutumika katika karibu sekta zote za kiuchumi.

Hatua ya Urusi kuvamia Ukraine tayari imechangia ongezeko la bei ya gesi ya kupikia kwa sababu bidhaa hii huzalishwa kwa wingi katika mataifa hayo mawili.

GESI YA KUPIKIA

Mnamo Jumatatu, kampuni ya Rubis Energy Kenya ilipandisha bei ya kujaza mitungi ya gesi kwa kiwango cha asilimia 15.

Hii ina maana kuwa bei ya gesi ya kilo sita sasa imepanda hadi Sh1,560 kutoka Sh1,400 nayo ya mtungi wa kilo 13 imepanda hadi Sh3,340 kutoka Sh2,800.

Pia, kuna uwezekano mkubwa kwamba bei ya bidhaa zinazotengenezwa kutokana na ngano, kama vile mkate, itapanda hivi karibuni.

Hii ni kwa sababu Kenya huagiza karibu asilimia 75 ya mahitaji ya ngano kutoka mataifa hayo mawili.

Urusi ndiyo inaongoza katika uuzaji nje wa ngano ulimwenguni ilhali Ukraine inashikilia nafasi ya nne katika biashara hiyo.Kando na ngano, Kenya pia huagiza bidhaa nyingine kama vile mbolea, chuma na mafuta ya kupikia kutoka Urusi. Bei ya bidhaa hizi inatarajiwa kuendelea kupanda ikiwa Rais Putin hatasitisha vita nchini Ukraine.

MBOLEA

Kwa mfano, msimu wa upanzi unapokaribia katika maeneo mengi nchini, bei ya mbolea aina ya DAP tayari imepanda na kufika Sh7,000 kwa gunia la kilo 50.

Aina hii ya mbolea ndio hutumia kwa wingi katika upanzi wa nafaka.

Wakulima wa Kenya nao wanakondolea macho hasara kubwa hasa wakuzaji wa majani chai, ikizingatiwa kuwa Urusi ni mojawapo ya mataifa ambayo hununua zao hili kwa wingi kutoka Kenya.

Kulingana na takwimu kutoka Shirika la Kitaifa la Takwimu Nchini (KNBS), Urusi ilinunua majani chai ya thamani ya Sh6.2 bilioni ya Kenya kuanzia Januari hadi Novemba 2021.

Kando na hayo, mataifa ya Urusi na Ukraine ni miongoni mwa mataifa ya Uropa ambako Kenya huuza parachichi kwa wingi.

Kulingana na takwimu kutoka Wizara ya Kilimo, Kenya iliuza parachichi za thamani ya Sh4.3 bilioni katika mataifa hayo kati ya Aprili na Novemba 2021.

Soko hili sasa limevurugwa na vita hivi.