Connect with us

General News

Pwani yawapa Raila na Ruto masharti makali – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Pwani yawapa Raila na Ruto masharti makali – Taifa Leo

Pwani yawapa Raila na Ruto masharti makali

Na BRIAN OCHARO

BAADHI ya viongozi wa kisiasa na wataalamu kutoka Pwani sasa wanawataka wakazi kuunga mkono wagombeaji wa urais ambao watahakikisha shughuli zote za bandari zinaendeshwa Mombasa.

Wakiongozwa na wabunge wa zamani, viongozi hao pia waliorodhesha masharti kadha ambayo wanataka yatimizwe na wagombeaji wa urais wanaotaka kura za eneo hilo.

Aliyekuwa Mbunge wa Malindi Lucas Maitha alisema eneo hilo litashirikiana na wagombeaji urais ambao watatia mkataba wa maelewano na vyama asili ya Pwani kama vile; Pan African Alliance (PAA), Umoja Summit Party, Kadu Asili na chama cha Shirikisho.

“Mkataba huo sharti uhusishe kurejeshwa kwa shughuli zote za bandari ikiwemo usafirishaji wa mizigo. Tutaunga mkono yule atakayetuhakikishia kuwa amri ya kuhamisha shughuli za bandari hadi maeneo mengine itafutiliwa mbali ndani ya siku 100 za mwanzo za uongozi wake,” Bw Maitha akawaambia wanahabari katika mkahawa mmoja jijini Mombasa.

Aliandamana na wabunge wa zamani; Thomas Mwadeghu (Wundanyi), Abdalla Ngozi (Msambweni), Willy Mtengo (Malindi) na mwenyekiti wa zamani wa chama cha walimu KNUT Mudzo Nzili.

Viongozi hao pia walisema wataunga mkono mgombeaji urais ambaye atawahakikishia, kwa maandishi, kwamba serikali yake itaanzisha hazina maalum ya kukusanya fedha za kuwapa makao mbadala maskwota.

“Kiongozi ambaye atatufaa ni yule ambaye atatushawishi kwamba atamaliza kabisa kero la uskwota katika eneo zima la pwani,” akasema Bw Maitha.

“Ikiwa kiongozi wa ODM Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto wanataka uungwaji kutoka kwetu, sharti wakubaliane na masharti yetu. Hatutamuunga mgombeaji yoyote kikasuku wakati huu,” akaongeza.

Viongozi hao walionya kwamba endapo mgombeaji mmoja wa urais atakataa masharti yao, ambayo yanajikita katika kufufua uchumi wa eneo hilo, basi wataunga mkono mgombeaji urais kutoka pwani.

“Tutaunga mkono mtu kutoka pwani hata kama atashindwa. Tutakuwa tumetoa msimamo wetu waziwazi kwamba tumechoka kutumiwa kisiasa kila mara,” akasema.

Aliyekuwa Mbunge wa Mwatate Calista Mwatela alisema eneo la pwani pia sharti litumie uwezo wake kujitetea kwa ajili ya kufaidi katika serikali ijayo.

Bw Mwatela alisema viongozi wa pwani sharti wazungumze kwa sauti moja ili wafaidi katika serikali itakayobuniwa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kustaafu mwaka huu.

“Maeneo mengine tayari yametoa masharti ambayo yangetaka yatimizwe kabla ya wakazi kuunga mkono wagombeaji fulani wa urais, Pwani haifai kuachwa nyuma,” akaeleza.

Viongozi hao pia waliunga mkono chama cha PAA kinachoongozwa na Gavana wa Kilifi Amason Kingi wakisema kinawakilisha maslahi ya wakazi wa eneo hilo.

Chama cha PAA tayari kimetangaza kuwa kinaunga mkono kiongozi wa ODM Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais.

Chama hicho pia kimejiunga na vuguvugu la Azimio la Umoja ambalo litageuzwa kuwa chama cha muungano mswada wa marekebisho ya sheria za vyama vya kisiasa ukiidhinishwa kuwa sheria.