Connect with us

General News

Raia wateseka siasa zikivuma – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Raia wateseka siasa zikivuma – Taifa Leo

Raia wateseka siasa zikivuma

Na CECIL ODONGO

WANASIASA wamezamia kampeni za mapema wakijiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 huku mamilioni ya Wakenya wakihangaika.

Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais Dkt William Ruto, Kinara wa ODM Raila Odinga na wanasiasa wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA) wamekuwa wakifanya misururu ya mikutano ya kujipigia debe huku wakionekana kutojali raia.

Kati ya changamoto zinazokumba Wakenya ni kupanda wa bei ya bidhaa hasa chakula, baa la njaa, kudorora kwa usalama, serikali kubomolea watu makazi kiholela, mvutano baina ya serikali na Bima ya Afya ya Kitaifa (NHIF) na tishio la ugaidi ambalo mataifa ya Magharibi tayari yameonya kuwa huenda likatekelezwa humu nchini.

Wakenya sasa watalazimika kutumia hela zao baada ya hospitali za kibinafsi kutangaza kuwa hazitakubali kadi za NHIF kuanzia Jumanne wiki ijayo.

Hospitali za kibinafsi zinapinga hatua ya serikali kupunguza ada ambayo imekuwa ikitozwa huduma mbalimbali za matibabu.

Idadi kubwa ya Wakenya wamekuwa wakitafuta huduma za matibabu katika hospitali za kibinafsi kwa kuwa hospitali za umma hukumbwa na uhaba wa dawa mara kwa mara.

Wabunge ambao wanafaa kushinikiza serikali kushughulikia mvutano huo wa NHIF, wamesalia kimya na wanasaidia vinara wao wa vyama kuendesha kampeni za kisiasa.

Kinaya ni kwamba katika mikutano yao ya kisiasa vigogo hao wamekuwa wakitoa ahadi za kuboresha afya na kuhakikisha mamilioni ya Wakenya wanajisajili kwa NHIF.

Mamilioni ya Wakenya katika maeneo mbalimbali nchini wanahitaji chakula kwa dharura kutokana na makali ya njaa.

Katika Kaunti ya Marsabit, kwa mfano, wakazi sasa wanalazimika kutembea kwa zaidi ya kilomita 40 wakitafuta chakula, maji na lishe kwa mifugo yao huku ukame ukiendelea kuwakeketa raia katika eneo hilo vibaya.

Aigus Nyemeto na familia yake ndani ya Manyatta yake katika eneo la Illeret, Kaunti ya Marsabit. Familia hiyo ni kati ya zilizoathiriwa pakubwa na njaa. PICHA | NICHOLAS KOMU

Maeneo yaliyoathirika vibaya ni eneobunge la North-Horr ambapo zaidi ya wakazi 200,000 wanahitaji chakula cha dharura kutokana na ukame wa muda mrefu.

Mizoga ya mifugo imezagaa kila mahali baada ya kufa kutokana ukosefu wa maji na nyasi.

Mbunge wa North Horr, Chachu Ganya jana Ijumaa aliambia Taifa Leo mtu mmoja amethibitishwa kufariki kutokana na makali ya njaa katika eneobunge lake.

Bw Ganya, hata hivyo, alikana kuwatelekeza wakazi wa eneobunge lake na kuzamia siasa.

“Niliwasilisha Bungeni hoja ya kuitaka serikali ishughulikie waathiriwa wa njaa. Sijakuwa nikifanya kampeni jinsi inavyodaiwa. Naendelea kushinikiza wizara ya Fedha na kuzungumza na mashirika mbalimbali ambayo sasa yanaendelea kupeleka msaada kuwaokoa wakazi. Kinachosikitisha ni kuwa hakuna mifugo kabisa kwa sababu ilikufa kutokana njaa na ukame huo,” akasema Bw Ganya.

Kinaya zaidi ni kuwa wanasiasa ambao wanatoka katika kaunti hizo za Kaskazini Mashariki ambazo zimeathiriwa sana kama vile mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale na Mwakilishi Mwanamke wa Garissa, Anab Subow ni kati ya wale ambao wamekuwa mstari wa mbele kuandamana na Naibu Rais Dkt William Ruto katika ziara zake za kusaka kura.

Katika Kaunti ya Lamu, kumekuwa na misururu ya mashambulio yanayodaiwa kutekelezwa na kundi la kigaidi la Al-Shabaab.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 20, wakiwemo maafisa wa polisi, wameuawa mwezi huu pekee katika Kaunti ya Lamu hasa vijiji vya Widho, Juhudi-Ukumbi, Marafa, Mashogoni, Milihoi na Bobo.Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i mapema Januari aliweka marufuku ya kutotoka nje katika tarafa nne za kaunti hiyo ila inaonekana kafyu hiyo haijasaidia katika kurejesha usalama mashambulizi yakiendelea kushuhudiwa.

Viongozi wanaotoka Kaunti ya Uasin Gishu na Trans Nzoia nao hawaonekani kujali masaibu ambayo wakulima wa mahindi wamekuwa wakipitia huku bei ya unga ikiendelea kupanda.

Ushuru wa asilimia 14 kwa pembejeo za kilimo ndio umetajwa kama sababu ya kupanda gharama ya uzalishaji.

Aidha kumekuwa na madai kuwa baadhi ya maafisa serikali wamekuwa wakishirikiana na wafanyabiashara kuagiza mahindi mengi kutoka taifa jirani la Uganda.

Kutokana na kujaa kwa mahindi sokoni, wakulima kutoka eneo hilo wamekuwa wakikosa soko la mazao yao huku baadhi ya kampuni za kusaga unga pia zikidaiwa zimekuwa zikihodhi mahindi kisha kununua yale yanayovunwa kwa bei ya chini.

“Ni wamiliki wa kampuni za kusaga unga ambao wamekuwa wakihodhi mahindi ili kusababisha upungufu. Lazima wachunguzwe kwa sababu wao wanaumiza Wakenya kwa kusababisha bei ya unga ipande,” akasema Katibu wa Cofek Stephen Mutoro.

Badala ya kushughulikia matatizo haya ya wakulima, wanasiasa wa Uasin Gishu wanaendelea kurindima ngoma ya Dkt Ruto huku wale kutoka Trans Nzoia wakigawanyika kuwili kwenye mirengo ya UDA na Azimio la Umoja.