Raila apata tikiti ODM kuwania urais mara 5
LEONARD ONYANGO na JURGEN NAMBEKA
KINARA wa ODM Raila Odinga sasa anaonekana kuwa na nguvu mpya huku akijiandaa kumenyana na mpinzani wake mkuu, Naibu wa Rais William Ruto katika kinyang’aniyiro cha urais Agosti 9.
Bw Odinga jana Ijumaa alijigamba kuwa hesabu aliyopiga 2018 kwa kuwatoroka wenzake wa muungano uliosambaratika wa NASA –Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Musalia Mudavadi (ANC) – na kutangaza kuungana na Rais Uhuru Kenyatta, inaelekea kuzaa matunda.
Bw Odinga aliwakejeli wapinzani wake waliodhani kuwa Rais Kenyatta angemsaliti kabla ya Agosti 9.
“Namshukuru Rais Kenyatta kwa kusalia mwaminifu kwangu na kutimiza tuliyoafikiana miaka minne iliyopita. Mimi na Rais tulikuwa mahasimu wakubwa. Baada ya uchaguzi wa 2017, tulikasirika na tukaambia wafuasi wetu kususia baadhi ya bidhaa zilizohusishwa na serikali ya Jubilee. Lakini mimi na Rais tukaona kuwa Wakenya ndio wanaumia na tukaweka chini tofauti zetu kwa manufaa ya nchi yetu ambayo ni kubwa kuliko sisi,” Bw Odinga alieleza viongozi wa ODM.
Rais Kenyatta pia amefanikiwa kuleta kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka katika kambi ya Bw Odinga – hatua ambayo itasaidia muungano wa Azimio la Umoja kuzoa kura nyingi eneo la Ukambani.
Bw Musyoka jana Ijumaa alisema wanalenga kuunda muungano utakaojulikana kama Azimio – One Kenya Alliance.
Vinara wa OKA wanatarajiwa kutia saini mkataba wa kukubali kuungana na Azimio Jumatatu.
Vyama vya Jubilee na ODM leo Jumamosi vitaidhinisha rasmi Bw Odinga kuwa mwaniaji wa urais wa muungano wa Azimio la Umoja.
Bw Odinga leo Jumamosi ataidhinishwa rasmi na wajumbe 3,000 wa ODM kuwa mwaniaji wa urais.
Hii ni baada ya Gavana wa Mombasa Hassan Joho na mwenzake wa Kakamega Wycliffe Oparanya ambao walikuwa wametuma maombi ya kutaka kuwania urais kujiondoa na kumwachia Bw Odinga.
“Siwezi kushindana na kiongozi wangu wa chama. Wewe ni kama baba yangu. Wewe ni kielelezo kwangu,” alisema Bw Joho alipotangaza kujiondoa kwenye mkutano wa viongozi wa chama (NGC) uliofanyika katika ukumbi wa Bomas.
Naye Rais Kenyatta, leo Jumamosi anatarajiwa kuongoza wajumbe 4,000 wa Jubilee katika Jumba la KICC kuidhinisha Bw Odinga kuwa mwaniaji wa urais.
Viongozi wa ODM na Jubilee walifaa kuandaa mkutano mkubwa katika uwanja wa Kamkunji jijini Nairobi kuzindua rasmi Bw Odinga kuwa mwaniaji wa urais wa Azimio la Umoja.
Mkutano huo, hata hivyo, umeahirishwa kwa wiki mbili ili kutoa fursa kwa viongozi wa OKA pamoja na vyama vinginevyo kutoka eneo la Mlima Kenya kujiunga na Azimio la Umoja.
Tofauti na mara nyingine nne ambazo amewahi kuwania urais, Bw Odinga anaamini mwaka huu atafaulu kuingia Ikulu. Kwa mara ya kwanza, Bw Odinga amepata uungwaji mkono kutoka kwa rais aliye mamlakani.
Hesabu ya Bw Odinga kutaka kuungwa mkono na Rais Daniel arap Moi mnamo 2002 haikufaulu baada ya kiongozi huyo wa pili wa Kenya kusema “Uhuru Kenyatta Tosha”.
Tangazo hilo la Moi lilighadhabisha Bw Odinga ambaye na wenzake waligura chama cha Kanu na kuunga mkono Mwai Kibaki ambaye aliibuka mshindi.
Next article
Kingi kuingia Azimio kupitia lango la Jubilee