[ad_1]
Raila kuzindua manifesto Jumatatu
NA LEONARD ONYANGO
MWANIAJI wa Urais wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga atazindua manifesto yake Jumatatu baada ya kuidhinishwa rasmi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Bw Odinga aliyekuwa akizungumza Jumanne alipokuwa akihutubia wanachama wa Baraza la Wafanyabiashara wa Ulaya (EBC) jijini Nairobi, alisema ataweka wazi mambo anayolenga kufanya ndani ya siku 100 iwapo atachaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.
Bw Odinga anatarajiwa kuwasilisha stakabadhi zake kwa IEBC Jumapili siku moja baada ya Dkt Ruto kuidhinishwa Jumamosi.
“Nitaelezea Wakenya mambo nitakayofanya ndani ya siku 100 baada ya kuchaguliwa Jumatatu baada ya kuwasilisha stakabadhi zangu kwa IEBC Jumapili. Sitafichua hapa,” Bw Odinga akaambia wafanyabiashara hao katika hafla ambayo pia ilihudhuriwa na mwaniaji mwenza wake Bi Martha Karua.
Bw Odinga amekuwa akijikokota kuzindua manifesto yake kutokana na madai kwamba baadhi ya ahadi zilizomo huenda zikanyakuliwa na mrengo wa Dkt Ruto.
Mwaniaji urais wa Azimio alipokuwa akizunguka katika kaunti za Mlima Kenya mwanzoni mwa Mei, aliahidi kuzindua manifesto yake baada ya wiki moja kuwezesha wagombea wanaotumia vyama tanzu vya muungano huo kuitumia kumvumisha katika maeneo ya vijijini.
Alipokuwa katika Kaunti ya Murang’a Mei 3, Bw Odinga aliwataka wawaniaji wa Azimio kutoogopa huku akiahidi kuwapa manifesto itakayowasaidia kushawishi wakazi wa eneo hilo.
Bw Odinga pia aliahidi kuwasaidia kifedha wawaniaji ambao watavumisha jina lake vijijini kwa kujumuisha picha yake katika mabango yao.
“Mfanye kampeni bila uwoga, tutawapa usaidizi wa kifedha na manifesto mtakayotumia kuendesha kampeni. Manifesto hiyo itazinduliwa wiki ijayo,” Bw Odinga akasema.
Naye, Dkt Ruto amekuwa akishutumu mrengo wa Bw Odinga kwa kunyakua baadhi ya ahadi zake ambazo amekuwa akizitoa.
[ad_2]
Source link