[ad_1]
Rais Kenyatta awasilisha bungeni majina ya watu 22 aliowateua kuwa mabalozi wapya
NA CHARLES WASONGA
SPIKA wa Bunge la Kitaifa ametangaza kupokea majina ya watu 22 walioteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuhudumu kama mabalozi wa Kenya katika mataifa mbalimbali ya nje.
Kwenye taarifa aliyoitoa Alhamisi, Mei 5, 2022, Spika Justin Muturi alisema kuwa majina ya watu hao yatasomwa rasmi mbele ya wabunge, mnamo Jumanne wiki ijayo.
Baadaye yatawasilishwa kwa Kamati kuhusu Ulinzi na Masuala ya Kigeni ambayo itaandaa vikao vya kuwapiga msasa kubaini ufaafu wao.
“Ningependa kuwajulisha wabunge kwamba mnamo Mei 4, 2022 nilipokea ujumbe kutoka kwa Mheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta kuhusiana na uteuzi wa watu 22 kushikilia afisi za mabalozi na wawakilishi wa Kenya katika mashirika ya kimataifa.
Kwa hivyo, kulingana na sheria za bunge nambari 42 (2) bunge litakaporejelea vikao vyake mnamo Mei 10, 2022, nitasoma ujumbe wa rais kwa wabunge, kisha majina hayo yatawasilishwa kwa kamati ya bunge kuhusu Ulinzi na Masuala ya Kigeni ili iwapige msasa,” Bw Muturi akasema.
Aliyekuwa Katibu katika Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) Bitange Ndemo ni miongoni walioteuliwa mabalozi. Ikiwa ataidhinishwa na bunge Profesa Ndemo atahudumu kama balozi wa Kenya nchini Ubelgiji.
Naye Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi, na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Profesa Richard Bosire ameteuliwa kuwa mwakilishi wa kudumu wa Kenya katika shirika la UNESCO.
[ad_2]
Source link