Rais Zelenskyy aapa kuendelea kupambana na Urusi
Na MASHIRIKA
KYIV, Ukraine
RAIS wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy jana Jumamosi aliapa kupambana vikali kulinda uhuru wa nchi hiyo huku wanajeshi wa Urusi wakifanya mashambulio kuelekea jiji kuu, Kyiv.
“Niko hapa. Hatutaweka silaha zetu chini. Tutalinda nchini yetu kwa sababu silaha zetu ndio ngao yetu,” akasema katika video iliyonaswa nje ya afisi yake jijini Kyiv na kusambazwa mitandaoni.
Rais Zelenskyy aliwataka raia wa nchi hiyo kupuuzilia habari za uwongo eti wanajeshi wa Ukraine wamekubali kusitisha vita.
“Habari nyingi feki zinasambazwa kupitia mtandao wa intaneti zikidai nimeamuru wanajeshi wetu kukomesha vita na kwamba shughuli za kuwaondoa raia maeneo hatari zimeanza,” akasema.
Huku akionekana mchovu lakini mkakamavu, akaongeza: “Ukweli ni kwamba hii ni ardhi yetu na nchi yetu, kwa hivyo tutailinda pamoja na watoto wetu. Hii ndio kile ambacho ningependa kuwaambia. Utukufu kwa Ukraine!”
Katika video ya awali, Rais Zelenskyy alikuwa ameliambia taifa hilo kusimama kidete huku akionya kuhusu uwezekano wa wanajeshi wa Urusi kushambulia Kyiv na miji mingine kote nchini humo.
“Huu utakuwa usiku mgumu kuliko mchana. Miji mingi inaelekea kushambuliwa. Miji ya Chernihiv, Samy, Kharkiv, Donbas na miji ya kusini wa Ukraine haswa Kyiv. Hatuwezi kupoteza jiji kuu,” Zelenskyy akasema Alhamisi jioni.
Kiongozi huyo alidai “mamia” ya wanajeshi wa Urusi wameauawa katika makabiliano hayo, lakini akaungama kuwa wanajeshi wa Ukraine pia wameuawa.
“Lengo letu kuu ni kukomesha umwagikaji wa damu. Adui amepoteza kwa kiwango kikubwa – wengi wa wanajeshi wao waliovuka mpaka na kuingia nchini mwetu wameuawa. Sisi pia tumepoteza wanajeshi wetu. Watu wa Ukraine watatumia kila mbinu kuzuia uvamizi huu ambao umefanywa bila sababu yoyote maalum,” akaongeza.
Zelenskyy pia alishutumu Urusi kwa kutumia roketi kushambulia majengo ya makazi, ikiwemo shule ya chekechea.
“Roketi zilipiga shule moja ya chekechea katika mji wa Vorzel jimbo la Kyiv. Roketi nyingine ziligonga mji wa Okhtyrka katika eneo la Sumy. Mbona watoto wa shule ya chekechea washambuliwe. Je, wao pia ni wanajeshi wa NATO ambao walitisha Urusi?” Rais huyo akauliza.
Uvamizi dhidi ya Ukraine ulianza Alhamisi asubuhi huku miji na vituo vya kijeshi vikishambuliwa kwa makombora yaliyorushwa na wanajeshi wa Urusi.
Mashambulio hayo ya angani yalifuatwa na yale ya ardhini yaliyohusisha wanajeshi wa Urusi walioko katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi ya Crimea na Belarus.
Rais Zelenskyy, ambaye awali aliomba usaidizi kutoka jamii ya kimataifa alisema alifanya mazungumzo na viongozi kadhaa wakiwemo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Rais wa Amerika Joe Biden.
“Tumekubaliana kuhusu misaada, usaidizi zaidi na usaidizi mkuu kwa taifa letu,” kiongozi huyo akasema.
Mnamo Ijumaa mataifa ya Amerika, Canada, Uingereza na Umoja wa Ulaya (EU) yalitisha kuiwekea vikwazo Urusi. Mataifa hayo pia yamemwekea vikwazo Rais wa Urusi Vladimir Putin na waziri wake wa masuala ya kigeni, Sergey Lavrov.