Ruto aghairi kubuni kituo kuhesabu kura
NA ONYANGO K’ONYANGO
NAIBU Rais William Ruto ameacha mpango wake wa awali wa kubuni kituo sambamba cha kuhesabia kura ili kulinganisha na matokeo yatakayokuwa yakitolewa kwenye vituo vya kupigia kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti.
Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2017, mwaniaji urais wa muungano wa Azimio La Umoja, Raila Odinga, alikuwa akidai kulikuwa na njama za wizi wa kura.
Hata hivyo, kufuatia handisheki kati yake na Rais Uhuru Kenyatta, Dkt Ruto sasa ndiye anayeonekana kuendeleza malalamishi hayo.
Dkt Ruto amekuwa akizielekezea lawama taasisi muhimu zinazotarajiwa kusimamia uchaguzi huo dhidi ya kupanga njama za kumwibia kura.
Ikiwa imebaki miezi minNe tu kabla ya uchaguzi huo kufanyika, muungano wa Kenya Kwanza—anaoongoza Dkt Ruto—unatoa malalamishi ambayo yalikuwa yakitolewa na uliokuwa muungano wa Nasa.
Muungano huo unatilia shaka kiwango ambacho Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imejitayarisha kuenedesha uchaguzi huo kwa njia ya uwazi.
Muungano vile vile umekuwa ukikosoa hatua ya Rais Kenyatta kuingilia mchakato wa urithi wake.
Unahisi kwamba huenda hali hiyo ikatia doa taratibu za maandalizi ya uchaguzi huo.
Hapo jana, mrengo huo ulisema kuwa hauna mpango wowote wa kubuni kituo kama hicho, ukisema badala yake, utawategemea maajenti wake kukusanya matokeo hayo kutoka vituo tofauti vya kupigia kura kote nchini.
Kulingana na Gavana Josphat Nanok (Turkana), ambaye ni miongoni mwa wasimamizi wa kampeni za Dkt Ruto, mrengo huo utahakikisha kuwa una maajenti wengi iwezekanavyo katika vituo vyote vya kupigia kura ili kulinda kura zao.
“Hatuna mpango wowote wa kubuni kituo cha kuhesabia kura. Hatuna mipango hiyo hata kidogo. Kikatiba, IEBC ndiyo inapaswa kuhesabu na kutoa matokeo rasmi,” akasema gavana huyo.
Akaongeza: “Kisheria, kuna viwango vitatu vya kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais. Hatua ya kwanza ni kuhesabu na kutangaza matokeo hayo katika kituo cha kupigia kura. Kuna afisa wa IEBC atakayefanya hivyo. Matokeo hayo yatakuwa rasmi na yatatolewa kwa yeyote, vikiwemo vyombo vya habari,” akasema Bw Nanok.
Alisema kuwa mrengo huo unapanga kujumuisha matokeo ambayo yatakuwa yametolewa na IEBC katika vituo vya kupigia kura na kutumwa kwao na maajenti wao.
Alisema kuwa hilo halipaswi kufasiriwa kama uwepo wa kituo sambamba cha kuhesabia kura.
Kile tutakachokuwa tukifanya ni kujumuisha matokeo kutoka kwa maajenti wetu. Tuna maajenti katika zaidi ya vituo 45,000 vya kupigia kura na vituo 24,000 vya kuhesabia matokeo. Jukumu letu litakuwa kulinganisha matokeo hayo ili kuhakikisha kuwa matokeo yanayotolewa na IEBC yanalingana na yale yaliyotolewa katika vituo vya kupigia kura na kiwango cha eneobunge,” akasema.
Next article
Mvutano wa Sossion, KNUT waelekezwa kwa uteuzi wa UDA Bomet