Ruto atoa onyo kwa asasi kuu za serikali
NA BENSON MATHEKA
NAIBU Rais William Ruto jana Jumanne aliidhinishwa rasmi kuwa mgombeaji urais wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) kwenye uchaguzi mkuu ujao na akatangaza kuwa, yuko tayari kuwakabili wapinzani wake katika muungano wa Azimio La Umoja.
Kwenye hotuba iliyosheheni hisia kali, Dkt Ruto aliwaahidi wapinzani wake ushindani wa aina yake akisema hatishwi na kuungana kwa vigogo wa kisiasa chini ya muungano wa Azimio La Umoja ambao unashirikisha wanasiasa maarufu kutoka pande zote za nchi.
Muungano huo ulimteua kinara wa ODM Raila Odinga kubeba bendera yake.
Unaleta pamoja vinara wa vyama vikubwa vya kisiasa akiwemo Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee, Kalonzo Musyoka (Wiper), Gideon Moi (Kanu), Charity Ngilu (Narc), Alfred Mutua (Maendeleo Chap Chap), Kiraitu Murungi (DEP), Peter Munya (PNU), Amason Kingi (PAA), Kivutha Kibwana (Muungano) na Jimmy Kibaki wa chama cha Young Democrats.
Vyama vingine ni United Progressive Party kinachohusishwa na Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i na Democratic Alliance Party of Kenya (DAP-K) kinachohusishwa na Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa miongoni mwa vingine.
Licha ya vigogo hao wa kisiasa na ushawishi wao kuungana dhidi yake, Dkt Ruto alisema hatishiki hata wakimpaka tope na kutumia vyombo vya usalama na uchunguzi kuhangaisha washirika wake.
“Ninataka kuwaambia niko tayari, sirudi nyuma na sitawaangusha kwa kazi ambayo mmenitwika siku ya leo,” akasema Dkt Ruto akihutubia wajumbe wa kitaifa wa chama cha UDA waliokutana uwanjani Kasarani, Nairobi.
Alisema huku wapinzani wake wakipanga kubadilisha katiba kubuni nafasi zaidi za kazi serikalini wagawane mamlaka, yeye atawajibika kuinua uchumi wa nchi akishinda urais ili masikini waacha kuteseka.
Alipokuwa akihutubu, wajumbe walilipuka kwa kuimba “Yote yawezekana bila Uhuru” hasa alipotaja jinsi idara za uchunguzi zinavyotumiwa kuhangaisha wabunge na wafanyabiashara wanaomuunga mkono.
Alionekana kumwelekezea kidole cha lawama Rais Kenyatta kwa kile alichodai kutelekeza ajenda za serikali zilizolenga kufaidi masikini na kuzingatia kutimiza maslahi ya kibinafsi.
Wajumbe wa UDA walimpa mamlaka ya kujadili, kuungana na kushirikiana na vyama au miungano mingine ya kisiasa kwa lengo la kushinda uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.
“Ninataka kuwafahamisha kwamba, niko tayari kwa jukumu ambalo mmenitwika leo. Nitazungumza na marafiki wetu ambao wamejiunga nasi leo kwa lengo la kuhakikisha tumetimiza lengo letu la kukomboa nchi yetu kutoka utumwa wa kiuchumi,” akasema.
Chama cha UDA kimekuwa kikishirikiana na Amani National Congress (ANC) cha aliyekuwa makamu rais Musalia Mudavadi na Ford Kenya kinachoongozwa na seneta wa Bungoma, Moses Wetangula ambao walihudhuria kongamano la Jumanne pamoja na William Kabogo wa chama cha Tujiebebe Wakenya, Moses Kuria wa Chama cha Kazi, Mwangi Kiunjuri wa The Service Party, Isaac Ruto wa Chama cha Mashinani (CCM)na Jimi Wanjigi wa chama cha Safina.
Huku akishangiliwa na wajumbe zaidi ya 5,000 waliomuidhinisha, Dkt Ruto alisema kampeni za UDA na washindani wake ni tofauti kama usiku na mchana.
“Wanatumia idara za serikali kuhangaisha washirika wangu ili kuwatisha na kuporomosha biashara lakini sisi tunalenga kuimarisha uchumi ili Wakenya wawe na pesa na kuishi maisha bora,” alisema.
Akichaguliwa rais, Dkt Ruto aliahidi kufanyia mageuzi Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Tume ya Maadili na Kubiliana na Ufisadi (EACC), Polisi na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA) akisema zimekuwa zikitumiwa kutimiza malengo ya kisiasa.
“Siku yangu ya kwanza nikiwa rais, nitafanyia mageuzi DCI na KRA ili ziache kutumiwa na maafisa wa serikali kutimiza maslahi ya kisiasa. Nitahakikisha DCI itafanya kazi yake kwa utaalamu na KRA itakusanya ushuru bila kunyanyasa na kuporomosha biashara za watu wasiokubaliana na walio mamlakani,” akasema Dkt Ruto.
Aliahidi kuimarisha sekta za kilimo, kuweka mfumo wa kupunguza madeni na kulinda uhuru wa Mahakama kwa kuitengea pesa zaidi. Alidai muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga ulitumiwa kunyima masikini maendeleo na kupandisha deni la kitaifa hadi Sh7 trilioni katika muhula wa pili wa serikali ya Jubilee.
“Tutachunguza deni hilo,” alisema.