Ruto kusalia Naibu hata akifurushwa Jubilee – Wataalam
Na CHARLES WASONGA
IMEBAINIKA kuwa Rais Uhuru Kenyatta anakabiliwa na kibarua kikubwa kumng’oa mamlakani naibu wake William Ruto licha ya Jubilee kutishia kumfurusha.
Wataalamu wa masuala ya sheria wanasema kuwa Dkt Ruto ataendelea kushikilia wadhifa huo hata kama atapokonywa cheo cha naibu kiongozi wa Jubilee au ajiuzulu kama mwanachama wa chama hicho tawala.
Jubilee imetangaza kuwa itaandaa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wake (NDC) mwishoni mwa mwezi huu wa Novemba kuidhinisha kuondolewa kwa Dkt Ruto na wandani wake.
Mapema wiki hii, Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Raphael Tuju, alisema kuwa chama hicho hakitaendelea kuwavumilia viongozi waasi ambao tayari wamekaidi sera na maongozi ya chama hicho na wanauza sera za chama pinzani cha United Democratic Alliance (UDA).
“Katiba ya chama chetu inasema wazi kwamba wale ambao wanaenda kinyume na sera zake watafurushwa. Hilo ni jambo muhimu zaidi kwa sababu kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Vyama vya Kisiasa, mtu hawezi kuwa mwanachama wa vyama viwili kwa wakati mmoja. Kwa hivyo, hatua hii muhimu ya kuwafurusha wakaidi itaidhinishwa katika NDC ambayo ni asasi yenye usemi wa juu zaidi katika Jubilee,” akawaambia wanahabari katika makao makuu ya chama hicho, Pangani, Nairobi.
Lakini kulingana na wakili Danstan Omari hatua hiyo haitamzuia Dkt Ruto kuendelea kushikilia wadhifa wa Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya kwa sababu afisi hiyo imelindwa na Katiba.
“Rais Kenyatta na wandani wake wanaweza kufaulu kumfurusha Dkt Ruto lakini atasalia kuwa Naibu Rais na kutumia rasilimali za umma katika kampeni zake za urais. Hii ni kwa sababu Rais hawezi kumfuta kwa sababu wawili hao walichaguliwa kwa tiketi moja,” anasema.
Kulingana na Bw Omari njia ya kipekee ambayo kwayo Dkt Ruto anaweza kupokonywa wadhifa huo ni kupitia hoja bungeni hatua ambayo itahitaji kuungwa mkono na thuluthi mbili ya idadi jumla ya wabunge (angalau wabunge 233).
“Hoja kama hiyo pia itahitaji kupata uungwaji mkono wa angalau maseneta 50 kati ya 67 kwa sababu hii ni afisi ya kikatiba,” akaeleza.
Itakuwa vigumu kwa hoja kama hiyo kupita bungeni wakati huu ambapo mirengo ya vyama vya Jubilee na ODM imegawanyika baada ya idadi kubwa ya wabunge wao kuviasi na kuunga mkono UDA.
Vile vile, nyakati hizi wabunge na maseneta wengi hukwepa kuhudhuria vikao vya mabunge hayo kwani wanatumia muda wao mwingi kuendesha kampeni za mapema kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.
Dkt Ruto ametangaza kuwa atawania urais kwa tiketi ya chama hiki katika uchaguzi mkuu ujao.
Awali, wabunge waaminifu kwa Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, wamejaribu kuandaa hoja ya kumtimua Dkt Ruto lakini juhudi zao zikagonga mwamba baada ya kung’amua kwamba haingepata uungwaji kutoka idadi tosha ya wabunge.
Katika mikutano yake ya kampeni Naibu Rais amekuwa akijigamba kuwa chama cha UDA kinaungwa mkono na zaidi ya wabunge 150 na zaidi ya maseneta 20.
Akiongea jana katika msururu wa kampeni katika Kaunti ya Bungoma, Dkt Ruto alidai kuwa kuna wabunge zaidi ambao wameahidi kujiunga na kambi yake ya “The Husler Nation” uchaguzi mkuu unapokaribia.