CHARLES WASONGA: Ruto na Raila wafafanue jinsi watakavyotekeleza ahadi zao
NA CHARLES WASONGA
NI bayana kwamba gharama ya maisha inaendelea kupanda kutokana na kuongezeka kwa bei ya bidhaa za kimsingi.
Kiwango cha madeni ya Kenya nacho kimefikia trilioni 8, kulingana na takwimu za hivi punde kutoka Benki Kuu ya Kenya (CBK).
Hii ina maana kuwa katika kipindi hiki cha kampeni, wagombeaji wa urais wanafaa kutoa matumaini kwa Wakenya.
Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga, ambao wanaonekana kuwa wagombeaji wenye ushawishi mkubwa wanafaa kufafanua sera na mifumo ya kiuchumi wanayonadi kwa raia.
Kwa mfano Dkt Ruto, katika mikutano yake ya kampeni amekuwa akiahidi kwamba serikali itatenga Sh100 bilioni kila mwaka za kutolewa kama mikopo ya kupiga jeki biashara za vijana ila huwa hasemi jinsi pesa hizo zitazalishwa.
Kwa mfano, sijawahi kumsikia Dkt Ruto akifafanua mikakati ambayo serikali yake itaweka kupunguza gharama ya uzalishaji bidhaa, kuimarisha biashara kati ya Kenya na mataifa ya kigeni na ile ya kupambana na jinamizi la ufisadi ambalo hufyonza karibu Sh600 bilioni kila mwaka.
Aidha, izingatiwe kuwa serikali imekuwa ikutimia karibu Sh1 trilioni katika bajeti yake ya Sh3.2 trilioni, kulipia madeni.Kwa upande wake Bw Odinga amekuwa akiendeleza “pambio” ya kuzipa familia maskini Sh6,000 kila mwezi pasina kusema jinsi serikali yake itazalisha fedha hizo.
Wapanga mikakati katika kambi ya Azimio la Umoja wanasema kuwa mpango huo utagharimu jumla ya Sh200 milioni kwa mwaka.
Lakini hawajafichua mbinu watakazotumia kutambua familia halali zinazohitaji ruzuku hiyo.
Pili, mpango wa Inua Jamii ambapo serikali huyapa makundi yenye mahitaji maalum, kama vile wakongwe na mayatima, Sh2,000 unayumba kutokana na kucheleweshwa kwa pesa hizo.