Ruto, Raila watumia jina la Kibaki kujiuza
NA MWANGI MUIRURI
NAIBU Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga wanatumia jina la rais wa tatu wa Kenya, Mwai Kibaki kujipendekeza kwa wapiga kura katika eneo la Mlima Kenya, Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 unapokaribia
Dkt Ruto anatumia suala la kuzorota kwa sekta muhimu zinazotegemewa na wakazi wa eneo hilo, hasa kilimo na biashara, kuwashawishi wapiga kura kwa ahadi kuwa akichaguliwa kwenye Uchaguzi Mkuu ujao ataimarisha uchumi wa eneo hilo jinsi ulivyokuwa wakati wa utawala wa Mzee Kibaki.
Mshirika wa Dkt Ruto katika muungano wa Kenya Kwanza, Musalia Mudavadi, ambaye duru zinasema ameahidiwa kuwa waziri wa fedha iwapo watashinda urais Agosti 9, amekuwa akiwaambia wakazi wa Mlima Kenya kila mara anapozuru eneo hilo kuwa atakuza uchumi hadi viwango ambavyo Kibaki alifanikiwa kuafikia.
Kwa upande wake, Bw Odinga amekuwa akieneza ujumbe kuwa alishirikiana kwa karibu na Kibaki katika kuzindua miradi yenye umuhimu wa kiuchumi kwa Mlima Kenya.
Kiongozi wa Wiper naye hajaachwa nyuma kutumia jina la Kibaki kujitafutia sifa eneo la Mlima Kenya kwani amekuwa akieleza mara kwa mara jinsi alimsaidia Kibaki mnamo 2007 wakati Bw Odinga alikuwa amekataa kukubali matokeo ya uchaguzi wa mwaka huo ambao ulisababisha ghasia za kikabila nchini.
Wachanganuzi wa siasa wanasema ingawa Mzee Kibaki ameaga dunia, ambapo shughuli ya umma kutazama mwili wake inaendelea katika majengo ya Bunge, utawala wake hasa kuhusu kuimarisha uchumi utasalia kuwa suala nyeti katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Kulingana na Bw Joseph Kaguthi, ambaye alihudumu katika utawala wa mikoa kwa muda mrefu, watu wa Mlima Kenya wanatumia utenda kazi wa Kibaki katika kupima rekodi ya Rais Uhuru Kenyatta, suala ambalo anasema linatumiwa kisiasa Uchaguzi Mkuu unapokaribia.
“Nimehudumu katika serikali kadhaa lakini hakuna rais yeyote anayeshinda Kibaki katika kujitolea kuboresha maisha ya watu. Watu wanatumia kigezo hiki kumhukumu Uhuru. Kwangu naona sio haki kwani wamehudumu katika nyakati na mazingira tofauti,” akasema Bw Kaguthi.
Lakini mshirika wa karibu wa Rais Kenyatta ambaye ni mbunge wa zamani wa Dagoretti Kusini, Dennis Waweru anatetea sera za uchumi za Rais Kenyatta akisema alipotwaa madaraka aliendeleza utimizaji wa ndoto ya Kibaki ya kuwa na taifa linaloheshimu demokrasia na raia wake wanaoishi maisha ya kuheshimika.
Bw Waweru anamtetea Rais Kenyatta akisema katika utawala wake amekumbana na changamoto nyingi kama vile Covid-19, mashambulio ya kigaidi ya Westgate, Dusit na maeneo ya Lamu na Kaskazini Mashariki pamoja na siasa za migawanyiko, lakini licha ya hayo amefanikiwa kukuza uchumi, kufanyia marekebisho sekta ya kilimo na kuimarisha miundo msingi.
Kulingana na takwimu za serikali, utajiri wa taifa umekua hadi Sh13 trilioni chini ya Rais Kenyatta ikilinganishwa na utajiri wa Sh5 trilioni alioacha Kibaki alipoondoka mamlakani 2013.
Lakini madeni mengi ambayo utawala wa Rais Kenyatta umekopa tangu 2013 yanafuta mafanikio hayo kwani mzigo wa deni sasa ni asilimia 66 ya utajiri wa Kenya ikilinganishwa na asilimia 46 aliyoacha Kibaki.
Umaskini pia umeongezeka chini ya utawala wa Rais Kenyatta kutoka asilimia 38 ya idadi ya Wakenya wakati Kibaki alipoondoka madarakani hadi asilimia 63 chini ya Jubilee.Seneta wa Tharaka Nithi, Kithure Kindiki anasema wengi wa wakazi wa Mlima Kenya wamevunjika moyo kutokana na kuzorota kwa hali yao ya kiuchumi chini ya utawala wa sasa.
Mbunge wa Kandara, Alice Wahome naye anasema rais alipoteza udhibiti wa ngome yake ya kisiasa ya Mlima Kenya kwa kupuuza masuala nyeti kwa wakazi hasa uchumi.
“Uhuru aliwasahau wale ambao walimpigia kura, na badala yake akawakumbatia waliokuwa wakimpinga. Hii ndiyo sababu wapiga kura wengi Mlima Kenya wanahisi ‘aliwasaliti’,” akasema.