Safari ya mwisho ya Kibaki yaanza rasmi
NA MARY WAMBUI
SAFARI ya mwisho ya rais wa tatu wa Kenya, marehemu Mwai Kibaki ilianza jana mwili ulipotolewa katika mochari ya Lee kwa msafara wa kijeshi hadi majengo ya Bunge kutazamwa na umma.
Jeneza lililokuwa na mwili wake lilibebwa kwa gari la kijeshi lililotumiwa kubebea jeneza la marehemu Daniel Moi mnamo Februari 2020.
Msafara wa kuusafirisha mwili huo ulilingana na ule ulioshuhudiwa wakati wa mazishi ya Mzee Moi.
Gari hilo la kijeshi linatengenezwa na kampuni ya Ateliers de Construction Mecanique de IÁtlantique (ACMAT) ambayo ina uhusiano na kampuni ya kutengeneza malori ya Renault Trucks Defence.
Kijigari hicho huwa kinatumika na jeshi kwa shughuli muhimu kama vile ukaguzi wa ufaafu wa maeneo ambako jeshi linalengwa kutumwa au kutekeleza shughuli zake.
Gari hilo huwa linatoa ulinzi maalum kwa walio ndani, kwani linaweza kuhimili shambulio la bomu.
Hata hivyo, gari hilo halijatumwa kushiriki kwenye vita vyovyote, bali limekuwa likitumika tu kwenye hafla za umuhimu wa kitaifa.
Msafara huo uliongozwa na Brigedia Jeff Nyagah, ambaye ndiye kamanda wa kikosi cha KDF kinachohudumu nchini Somalia.
Kisadfa, Brigedia Nyagah pia aliongozwa gwaride la mwisho la kijeshi kukaguliwa na Bw Kibaki mnamo Aprili 9, 2013, wakati alikabidhi mamlaka kwa Rais Uhuru Kenyatta katika Uwanja wa Michezo wa Kasarani.
Msafara huo pia uliwabeba maafisa tisa wa ngazi za juu wa kiwango cha Kanali wakiwa wamevaa mavazi ya kijeshi mekundu.
Upekee wa msafara huo uliwavutia Wakenya wengi ambao walijitokeza barabarani kuutazama huku wengine wakipiga picha kwa simu zao za mikononi.
Mwendo wa saa moja na robo asubuhi, msafara huo ulifika katika Bunge, ambapo jeneza hilo liliwekwa kwenye kijigari maalum.
Baadaye, jeneza hilo lilielekezwa ndani ya Bunge, likisindikizwa na makanali 10 na viongozi wachache wa kidini.
Baada ya hapo, mwili wa Bw Kibaki uliondolewa kutoka jeneza na kuwekwa kwenye meza maalum ili kutazamwa na umma.
Rais Uhuru Kenyatta ndiye aliyekuwa wa kwanza kuutazama.
Msafara wake ulifika Bungeni mwendo wa saa nne asubuhi.
Makanali hao wataulinda mwili huo kwa zamu kwa muda wa siku tatu ambao utatazamwa na umma.
Kwa siku hizo tatu, Brigedia Nyagah ndiye atakuwa akiongoza msafara huo katika kuupeleka bungeni na kuurudisha katika mochari ya Lee nyakati za jioni.
Marehemu Kibaki atazikwa nyumbani kwake eneo la Othaya, Kaunti ya Nyeri hapo Jumamosi.