Salah, Elneny na Trezeguet kuongoza Misri katika fainali za AFCON nchini Cameroon
Na MASHIRIKA
MAHMOUD Ahmed Ibrahim Hassan almaarufu Trezeguet amejumuishwa katika kikosi kitakachotegemewa na Misri kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Cameroon kuanzia Januari 9 hadi Februari 6, 2022.
Mshambuliaji huyo wa Aston Villa ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ameitwa kambini mwa Misri licha ya kutocheza mechi yoyote ya haiba tangu Aprili 2021.
Trezeguet, 27, alifanyiwa upasuaji wa goti baada ya kupata jeraha alipokuwa akichezea Villa katika EPL mnamo Aprili 10, 2021. Jeraha hilo lilimkosesha fursa ya kuchezea Misri mechi zote sita za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazoandaliwa nchini Qatar mnamo 2022.
Mnamo Disemba 6, 2021, Trezeguet alipangwa katika kikosi cha chipukizi wa wasiozidi umri wa miaka 23 kambini mwa Villa na akafunga bao. Tangu wakati huo, amekuwa akipangwa katika kikosi cha akiba cha Villa katika mechi tatu zilizopita bila ya kuchezeshwa.
Jinsi ilivyotarajiwa, kocha Carlos Queiroz amemjumuisha pia kikosini nyota matata wa Liverpool, Mohamed Salah ambaye atakuwa nahodha wa Misri akisaidiwa na kiungo mahiri wa Arsenal, Mohamed Elneny.
Wanasoka wengine wanaochezea ughaibuni ambao kocha huyo msaidizi wa zamani wa Manchester United amewaita kambini mwa Misri ni Ahmed Hegazi (Saudi Arabia), Mostafa Mohamed (Uturuki) na Omar Marmoush (Ujerumani).
Misri ambao ni mabingwa mara saba wa AFCON wameratibiwa kuanza kampeni zao za makala yajayo dhidi ya Nigeria mnamo Januari 11 kabla ya kuvaana na Guinea-Bissau kisha Sudan.
KIKOSI CHA MISRI KWA AJILI YA AFCON:
Makipa: Mohamed El-Shennawy (Al Ahly, Misri), Mohamed Sobhi (Pharco, Misri), Mohamed Abogabal (Zamalek, Misri), Mahmoud Gad (Enppi, Misri).
Mabeki: Ahmed Fatouh, Mahmoud Alaa, Mahmoud Hamdy El-Wensh (wote wa Zamalek, Misri), Ayman Ashraf, Akram Tawfik, (wote wa Al Ahly, Misri), Omar Kamal, Mohamed Abdel-Moneim (wote wa Future, Misri), Ahmed Hegazi (Ittihad Jeddah, Saudi Arabia).
Viungo: Hamdi Fathi, Amr El-Sulya (wote wa Al Ahly, Misri), Emam Ashour, Ahmed Sayed Zizo (wote wa Zamalek, Misri), Abdallah El-Said, Ramadan Sobhi (wote wa Pyramids, Misri), Mohamed Elneny (Arsenal, Uingereza), Omar Marmoush (VfB Stuttgart, Ujerumani), Mohanad Lasheen (Tala’a El-Gaish, Misri), Mahmoud Hassan Trezeguet (Aston Villa, Uingereza).
Mafowadi: Mostafa Mohamed (Galatasaray, Uturuki), Mohamed Sherif (Al Ahly, Misri), Mohamed Salah (Liverpool, Uingereza).
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO