Seneta Ledama Olekina kuwasilisha kesi mahakamani kupinga kufutwa kazi kwa wafanyakazi wa Kemsa
Na CHARLES WASONGA
SENETA wa Narok Ledama Olekina amepinga kile anachodai ni mpango wa Mamlaka ya Usambazaji Dawa Nchini (KEMSA) kuwafuta kazi jumla ya wafanyakazi 900 wa mamlaka hiyo inayozongwa na sakata za ufisadi.
Akiongea na wanahabari katika majengo ya bunge Novemba 4, 2021, seneta huyo alisema sio haki kwa wafanyakazi hao kufutwa kazi ilhali wakuu wa mamlaka hiyo waliohusishwa na sakata ya Sh7.8 bilioni katika ununuzi wa bidhaa za corona wanaendelea kupokea nusu ya mishahara yao.
“Nitawasilisha kesi mahakamani kutetea wafanyakazi hawa masikini ikiwa Bunge la Kitaifa na Seneti hazitasitisha hatua hii ya Kemsa. Hii ni kwa sababu hatua hiyo inakiuka haki za kisingi za wafanyakazi hao pamoja na sheria husika,” Bw Olekina akaongeza.
Seneta huyo pia alidai kuwa amepata habari kwamba wafanyakazi hao wa ngazi za chini wanafutwa kazi kama sehemu ya mpango wa kuweka Kemsa chini ya usimamizi wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF).
“Kuna haja gani ya kuweka asasi hii chini ya usimamizi wa jeshi ilhali maafisa wake walioiba fedha za umma kupitia sakata ya ununuzi wa vifaa vya kupambana na corona hawajaadhibiwa. Hii ni licha ya Rais Uhuru Kenyatta mwaka 2020 kutoa makataa ya siku 21 kwa asasi husika kuwafungulia mashtaka wahusika katika sakata hiyo,” Bw Olekina akaongeza.
Muda mfupi baada ya Seneta huyo kutoa madai hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Kemsa Bi Chao Mwadime aliamuru kuwa wafanyakazi wa ngazi ya chini ya mamlaka hiyo wafanye kazi kutoka nyumbani kwa siku 30.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari mwenyekiti huyo alisema hatua hiyo ambayo itaanza kutekelezwa kuanzia Novemba 5, 2021 imechukuliwa ili kutoa nafasi kwa utekelezaji wa mageuzi katika Kemsa.
“Wasimamizi wa muda watafuatilia utendakazi wa wafanyakazi hao kwa kipindi kilichowekwa katika notisi hii. Ushauri nasaha na usaidizi hitajika wa kisaikolojia utatolewa kwa wafanyakazi wote,” Bi Mwadime akaongeza.
Mwenyekiti huo alisema kuwa mageuzi katika Kemsa yalipendekezwa kamati ya maalum iliyoteuliwa na bodi yake kuchunguza changamoto zinazoikabili na hivyo kuizuia kutekeleza majukumu yake.
“Katika ripoti yake iliyowasilishwa kwa bodi ya Kemsa, kamati hiyo ilibaini changamoto kadha zinazoizuia kutimiza mahitaji ya wateja wake. Mahitaji hayo ni kama vile dawa na bidhaa nyingine za kimatibabu kwa serikali za kaunti na hospitali za rufaa,” akasema Bi Mwadime.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa hali hiyo imehatarisha maisha ya Wakenya na kuhujumu mpango wa Serikali wa Afya kwa Wote ifikapo mwaka wa 2022.
“Kwa hivyo mageuzi haya yataweka msingi wa kufikinishwa kwa malengo ya Ajenda Nne Kuu za Maendeleo ya Serikali, hususan kufanikishwa kwa mipango na Afya kwa Wote,” Bi Mwadime akaongeza.
KEMSA iligonga vichwa vya habari mwaka 2020 kufuatia kufichuliwa kwa sakata ya ununuzi bidhaa za kutumika kama vita dhidi ya Covid-19 kinyume cha sheria na kwa bei ya juu kupita kiasi.
Bidhaa hizo zilizojumuisha barakoa na magwanda ya kutumiwa na wahudumu wa afya kujikinga dhidi ya maambukizi (PPE) zilikuwa na thamani ya Sh7.8 bilioni.
Bunge na asasi nyingine zilizochunguza sakata hiyo ziligundua kuwa zabuni ya ununuzi wa bidhaa hizo ilitolewa bila idhini ya afisi husika katika Kemsa na Wizara ya Afya.
Baadhi ya kampuni zilizopewa zabuni ya thamani ya mabilioni ya fedha hazikuwa zimehitimu wala kutimiza masharti ya sheria kuhusu ununuzi wa bidhaa za umma.
Kufuatia sakata hiyo, aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Kemsa Jonah Manjari alisimamishwa kazi, kwa muda, kwa tuhuma za kukiuka sheria wakati wa utoaji wa zabuni za ununuzi wa bidhaa hizo za kupambana na corona.
Wengine waliosimamishwa kazi baada ya kunyoshewa kidole cha lawama katika sakata hiyo ni Mkurugenzi wa Idara ya Ununuzi Charles Juma na Mkurugenzi wa Huduma za Kibiashara Eliud Mureithi.