Connect with us

General News

Seneti yapitisha mswada tata wa vyama vya kisiasa licha ya pingamizi kutoka kwa wandani wa Dkt Ruto – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Seneti yapitisha mswada tata wa vyama vya kisiasa licha ya pingamizi kutoka kwa wandani wa Dkt Ruto – Taifa Leo

Seneti yapitisha mswada tata wa vyama vya kisiasa licha ya pingamizi kutoka kwa wandani wa Dkt Ruto

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta sasa anaweza kutia saini mswada tata wa marekebisho ya sheria za vyama vya kisiasa wakati wowote baada ya maseneta kuupitisha Jumatano usiku bila kuufanyia marekebisho yoyote.

Katika kura ya mwisho iliyopigwa kubaini hatima ya marekebisho kadha yaliyowasilishwa na maseneta wandani wa Naibu Rais William Ruto, wandani wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga waliibuka washindi.

Jumla ya maseneta 29 walipiga kura ya kuunga mkono mswada huo jinsi ulivyopitishwa kutoka Bunge la Kitaifa ilhali maseneta saba waliupinga.

Maseneta wanaogemea chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Dkt Ruto walifeli katika juhudi zao za kusambaratisha mswada huo wenzao wa ‘handisheki’ walipofaulu kutupilia mbali hoja 16 za marekebisho ya vifungu vyake kadha.

Miongoni mwa maseneta waliowasilisha hoja za marekebisho kwa mswada huo ni pamoja na; Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Samson Cherargei (Nandi), Petronila Were (Seneta Maalum), Irungu Kang’ata (Murang’a), Isaac Mwaura (Seneta Maalum) na Enock Wambua (Kitui).

Bw Murkomen alisema japo mswada huo ulipita, yeye na wenzake waliupinga na wataendelea kuupinga katika majukwaa mengine.

“Kuna sehemu mbalimbali katika mswada huu zinazokiuka Katiba. Aidha, utaratibu ufaao haukufuatwa wakati wa utayarishaji wa mswada huu. Hata kama wameupitisha, tutakutana mbele,” seneta huyo wa Elgeyo Marakwet akasema.

Mjadala kuhusu mswada huo uliokumbwa na kelele nyingi ulidumu kwa zaidi ya saa saba katika kikao hicho maalum kilichoitishwa mahususi kushughulikia ajenda hiyo.

Kiongozi wa wachache James Orengo alipongeza kupitishwa kwa mswada huo akisema utaimarisha mipango ya vyama kubuni miungano kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

“Ningependa kupongeza maseneta wenzangu kwa kupitisha mswada huu muhimu unaotoa mwongozo utakaowezesha kuundwa kwa miungano ya vyama na kuviwezesha kuendesha shughuli zao kwa amani bila misukosuko ambayo ilizonga miungano miaka ya nyuma.” akasema seneta huyo wa Siaya.

Awali, mnamo Jumanne, Januari 25, 2022 Kamati ya Seneti Kuhusu Sheria chini ya uongozi wa Seneta wa Nyamira Okong’o Omogeni iliwasilisha ripoti iliyopendekeza kuwa mswada huo upitishwe bila kufanyiwa marekebisho.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending