Connect with us

General News

Serikali iepuke mvutano na Miguna Miguna – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Serikali iepuke mvutano na Miguna Miguna – Taifa Leo

TAHARIRI: Serikali iepuke mvutano na Miguna Miguna

Na MHARIRI

MWANAHARAKATI na Wakili aliye na makao nchini Canada, Miguna Miguna hatimaye ametangaza kuwa yupo njiani anarejea nchini baada ya kuwa ‘uhamishoni’ tangu 2018.

Ni jambo ambalo limezua hisia mseto haswa ikikumbukwa mazingira ambayo wakili hiyo alijipata kupakiwa kwenye ndege na kusafirishwa hadi Canada huku majaribio yake ya kurejea nchini yakizimwa na asasi za serikali mara kadhaa licha ya maagizo ya mahakama.

Miguna aliandamwa na serikali punde tu baada ya kushiriki zoezi lililopingwa na serikali, la kumuapisha Kinara wa NASA wakati huo Raila Odinga kuwa Rais wa Wananchi, baada ya kukataa kushiriki marudio ya uchaguzi kufuatia Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2017 kufutiliwa mbali na Mahakama ya Juu.

Vuta nikuvute ikaanzia hapo huku Miguna akitoa cheche za maneno kukashifu serikali ya Uhuru Kenyatta na mwenzake kwenye maridhiano (Handshake) Bw Odinga na yeyote yule aliyepingana naye kwenye safu za mitandao ya kijamii.

Lakini sasa, Bw Miguna amesema yupo njiani na anatazamia kuwasili kesho Jumanne baada ya kupambana mahakamani ili kuondolea mbali marufuku ya kutokanyaga nchini (red alert) iliyokuwa imewekwa na serikali.

Kulingana na Wakili wake Nelson Havi, uamuzi uliotolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Hedwig Ong’udi mnamo Ijumaa, unasema kwamba serikali imethibitisha kwamba haimzuii Miguna kuingia Kenya.

Awali, Jaji Mkuu mstaafu Willy Mutunga alikuwa akipanga kwenda Canada ili aje na Miguna lakini viza yake ilichelewa kuandaliwa hivyo basi akakosa kusafiri.

Kile Wakenya wengi wanachotaka kuona ni Bw Miguna, aliye mzawa wa taifa hili, akiruhusiwa kurudi nyumbani bila vikwazo vyovyote wala ghasia endapo ametimiza hitaji la stakabadhi za usafiri ambazo kila mtu huhitajika kuwa nazo.

Haitakuwa picha nzuri hata kidogo kuona tena hali ya mshikemshike baina ya polisi au maafisa wa uhamiaji na wakili huyu hata ingawa huzungumza mambo wasiyopenda kusikia.

Ukomavu wa serikali yoyote hudhihirika kwa kuangalia jinsi inavyokabiliana na wakosoaji wake.

Bw Miguna ana haki yake ya kidemokrasia kuzungumza na kukosoa, pamoja na kutembelea nchi yake ya kuzaliwa kama watu wengine.

Na kwa jinsi serikali ilivyokashifiwa mnamo 2018 ilipomvuruga wakili huyo licha ya maagizo mengi ya mahakama iliyoizuia kufanya hivyo, hii hapa fursa yajitokeza kwa serikali kufanya haki na kumruhusu Bw Miguna kurudi nyumbani.