TAHARIRI: Serikali ifuate sheria katika mageuzi ya CBC
Na MHARIRI
WIZARA ya Elimu haiwezi kutangaza mambo muhimu yanayowahusu watoto bila ya kushirikisha umma kwenye Mfumo wa elimu wa Umilisi (CBC).
Hatua ya Waziri Prof George Magoha kutangaza kwamba watoto watakaojiunga na shule za Sekondari za Awali watagawanywa katika vitengo vitatu, inafaa lakini ugawaji shule zitakazohusika lazima ujadiliwe.
Kwenye mpango huo, wanafunzi wa CBC watagawanywa katika mapote matatu.
Kuna wanafunzi watakaosomea Sanaa na Michezo; kundi la pili (Sayansi ya Jamii); na ka Tatu (Sayansi , Teknolojia, Uhandisi na Hisabati).
Serikali inasema shule za mashambani, za kutwa na zisizo na vifaa vya kutosha zitafunza kundi la kwanza na la pili la masomo hayo.
Zile za bweni na zenye vifaa zitafunza makundi yote matatu.
Kile ambacho serikali haijafafanulia wazazi ni jinsi ambavyo wizara ya Elimu itakavyoamua kuhusu watoto kusoma aina fulani ya masomo.
Kama kwa mfano mtoto atakuwa mzuri kwa Sanaa na Michezo na pia masomo ya Hisabati lakini akose shule yenye vifaa, itakuwaje?
Kwenye mpango huo wa watoto watakaomaliza Gredi ya Sita watajiunga na shule hizo.
Ndio maana waziri wa Elimu amekuwa akizunguka nchi nzima kuhakikisha kuna madarasa 10,000 kabla ya wanafunzi walio Gredi ya Tano kujiunga na Gredi ya Sita baadaye mwezi Aprili.
Mambo mawili lazima yawekwe wazi.
Kwanza mtoto wa Gredi ya Saba ana umri wa kati ya miaka 11 na 12. Huyo si mtu anayeweza kujisimamia katika baadhi ya mambo.
Iwapo ataitwa kwenye shule za mbali na kwao, kutakuwa na mipango gani kuhakikisha wanajisimamia?
La msingi, mfumo wa CBC kwanza ungekuwa na masomo ya kuwafunza watoto kufua nguo, kuosha vyombo, kuweka vyema vifaa vyao muhimu kati ya mambo ya msingi ya kuwawezesha kujitegemea.
Pili, tumeshuhudia visa vingi vya mijengo kuporomoka. Sababu kubwa ya mikasa hii ni ujenzi kuharakishwa. Serikali imeonekana ikirudia kosa hilo kwa kuwasukuma vibarua kujenga madarasa kwa kasi ya ajabu.
Kuna uhakika gani kwamba madarasa hayo yanayojengwa kwa ajili ya wanafunzi wa Sekondari ya Chini hayatawaporomokea? Swali hili huenda lisieleweke kwa sasa, lakini ipo siku matokeo ya mbio hizi yataonekana peupe.
Elimu ni sekta muhimu ambayo maamuzi kuihusu hayafai kusimamiwa na serikali pekee bila ya kuwashirikisha wadau, hasa wazazi.
Next article
Pigo kwa taaluma ya Kiswahili mtaalam akifariki