JUMA NAMLOLA: Serikali itumie maneno matamu kushawishi watu wachanjwe
Na JUMA NAMLOLA
MAWASILIANO ni taaluma inayofungamana na kila sehemu ya maisha ya mwanadamu.
Waataalamu wa masuala ya mawasiliano, wanasema hakuna mwanadamu asiyeweza kuwasiliana.
Kusema ni kuwasiliana, na kunyamaza pia ni kuwasiliana.
Kwa kuwa kila mtu huelewa jambo kulingana na mtazamo wake, itikadi yake, mazingira aliyokulia na kadhalika, mtu anayetaka kuwasiliana ni lazima aunde ujumbe ambao utafasiriwa vile alivyoudhamiria.
Wizara ya Afya ina idara nyingi na maafisa wengi wa mawasiliano.
Ilitarajiwa wangewashauri mabosi wao kuhusu jinsi ya kuwasiliana na umma.
Mojawapo ya mambo ambayo serikali (wizara ya Afya) imefeli kabisa kuyaeleza kwa wananchi kwa njia rahisi, ni umuhimu wa watu kuchanjwa.
Wakuu wa mawasiliano katika wizara, walimruhusu waziri Mutahi Kagwe (aliyewahi kuwa waziri wa Habari na Mawasiliano) kutumia vitisho katika uenezaji habari kuhusu corona, vipimo na chanjo.
Vitisho ni sehemu tu katika mambo sita yanayoangaziwa na wataalamu wa mawasiliano kuhusu afya, wanapotaka mtu abadilike kuhusiana na maradhi.
Anayetarajiwa kurekebisha tabia, pia hutakiwa aelewe faida ya kujiepusha na jambo au kulifanya na kadhalika.
Msimamo wa Kanisa Katoliki kuikemea wizara ya Afya kwa kusema serikali itanyima huduma wasiochanjwa dhidi ya corona, uko sahihi.
Kufikia sasa ni watu wasiozidi milioni tisa waliochanjwa. Kati ya hao, milioni tatu pekee ndio waliopata chanjo zote mbili.
Hii ni chini ya asilimia 10 ya Wakenya wote.
Serikali inaposema wasiochanjwa hawatapewa huduma katika afisi za umma, ina maana gani?
Ina maana kuwa wafanyikazi katika afisi za serikali watakuwa wakikaa tu bure na kupokea mishahara mwisho wa mwezi?
Hao watu milioni nane waliochanjwa, si wote huingia katika afisi za serikali kila siku kutafuta huduma.
Badala ya kuwanyima huduma, serikali ingetengeneza ujumbe kushughulikia uzushi ambao watu wanaambiwa kuhusu chanjo.