Connect with us

General News

Serikali iwasake wanaoendesha uuzaji haramu wa vyuma vikuukuu – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Serikali iwasake wanaoendesha uuzaji haramu wa vyuma vikuukuu – Taifa Leo

TAHARIRI: Serikali iwasake wanaoendesha uuzaji haramu wa vyuma vikuukuu

NA KITENGO CHA UHARIRI 

UAMUZI wa Rais Uhuru Kenyatta kupiga marufuku kwa muda biashara ya vyuma vikuukuu unastahili pongezi.

Biashara hiyo imechangia visa vya wizi na ajali barabarani. Kulingana na Rais Kenyatta, baadhi ya wafanyibiashara wasiojali walifungua vyuma vya nyaya za kusambaza nguvu za umeme eneo la Naivasha. Wengine hata hujaribu kuuza vyuma vya milingoti ya mawasiliano.

Taifa Leo mara kadhaa imewahi kufichua visa ambapo, magari yanayoibwa Nairobi huishia kwenye gereji za watu wanaozichanja kwa shoka kama kuni na kuuza spea zake.

Ni majuzi tu ambapo watu fulani walijaribu kuiba vyuma vya reli ya SGR eneo la Makueni.

Waendeshaji biashara hiyo, ambapo idadi kubwa hawana leseni, wamekuwa wakijali faida wanayopata kuliko usalama wa wananchi.

Kwa mfano mabango kwenye barabara yanayoonyesha kwa mfano, kuna daraja mbele au usipitishe mwendo wa kilomita fulani kwa saa, hung’olewa na kuuza kama skrepu.

Matokeo yake ni kuwa, huenda dereva anayetumia barabara kwa mara ya kwanza, akatumbukia mtoni au akasababisha ajali kwa kwenda kasi kuliko inayotakikana.

Kwenye barabara nyingi ambako wanyamapori huvuka, huwa kuna mabango ya kuonyesha maeneo husika. Inakuwaje kukikosekana mabango hayo na wanyama wavuke barabara ghafla?

Serikali kupitia Bunge mwaka 2015 iliunda sheria iliyobuni Baraza la Vyuma Vikuukuu nchini (SMC) kwa lengo la kudhibiti sekta hiyo nchini.

Kulingana na sheria hiyo, mtu anayepatikana na hatia ya kuuza, kununua au kutengeneza vifaa vinavyotokana na vyuma hivyo bila leseni, atatozwa faini ya fedha zisizozidi Sh200,000 au kifungo cha miezi mitatu gerezani.

Swali linalotatiza Wakenya wengi ni; inakuwaje maafisa wenye jukumu la kufuatilia utekelezaji sheria waliacha biashara hii kuendelea? Mbona wakuu wa Mamlaka ya Barabara Kuu nchini (KeNHA) haijawatoza faini ya Sh500,000 wanaoiba vyuma vya kando ya barabara?

Mbali na Rais Kenyatta kusimamisha biashara hii ya vyuma, serikali pia yapaswa kuwakamata wasimamizi wa idara husika. Baadhi ya maafisa wa polisi na wale wa SMC huwa wanajuana na wanaoendesha biashara kwa njia haramu.

Wakati huu ambapo serikali inapanga kufanyia marekebisho idara inayosimamia biashara hiyo, ni sharti watu wakamatwe na kuadhibiwa.

Haiwezekani kwamba hatua pekee itakuwa kusimamisha biashara na baadaye uharibifu uendelee.