Connect with us

General News

Serikali ya Ethiopia iko hatarini kupinduliwa – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Serikali ya Ethiopia iko hatarini kupinduliwa – Taifa Leo

MUTUA: Serikali ya Ethiopia iko hatarini kupinduliwa

Na DOUGLAS MUTUA

UKITAKA kujua serikali imelemewa na waasi wakati wa vita, amiri jeshi mkuu huwahimiza raia wa kawaida watwae silaha na kujilinda.

Hilo ndilo tamko alilotoa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Dkt Abiy Ahmed, hivi majuzi waasi wa Tigray People’s Liberation Front (TPLF) walipotangaza kulinusa jiji la Addis Ababa.

Sasa taifa hilo lililo la pili kwa wingi wa watu barani Afrika limegubikwa na hofu kwani kiongozi huyo ametangaza hali ya hatari pia!

Tangazo la hali ya hatari lina maana kwamba jeshi la Ethiopian People’s Defence Forces (EPDF) linaweza kuwaingiza vijana jeshini bila hiari yao ili kushiriki vita hivyo.

Na kila mkazi wa jiji la Addis Ababa aliye na silaha, halali au haramu, ameagizwa aisajili rasmi kwa serikali ili atambuliwe kama mpambanaji dhidi ya waasi wa TPLF.

Waasi hao walidai wanaweza kuingia Addis Ababa kwa mshindo walipoitwaa miji ya Dessie na Kombolcha iliyo kaskazini mwa taifa hilo na kuwafukuzia mbali wanajeshi.

Kutekwa kwa Kombolcha hasa kumempa hangaiko Dkt Ahmed kwa kuwa uko kwenye barabara ya kuelekea Addis Ababa.

Tayari barabara hiyo imefungwa asipenye adui yeyote kuingia jiji hilo ambalo limezungukwa na waasi wengine, Oromo Liberation Army (OLA), wanaoazimia kulitwaa.

Serikali imepambana na TPLF tangu Novemba 2020 kwa kutoelewana kisiasa huku pia ikiwalaumu kwa kushambulia kambi ya jeshi iliyokuwa eneo la Tigray.

Kioja kikuu ni kwamba TPLF ndiyo iliyokuwa chama tawala nchini humo wakati wa utawala wa aliyekuwa waziri mkuu, Meles Zenawi, hadi alipofariki.

Vyama vingine vilivyoshirikiana nayo kuongaza nchi viliihujumu na kuipokonya vyeo muhimu Meles alipofariki, lakini iliendelea kuiongoza serikali ya Jimbo la Tigray.

Vyama hivyo vilichukua hatua hiyo kwani marehemu alikuwa ameidhibiti nchi kwa kuwajaza watu wa kabila lake, Tigray, katika kila ngazi ya uongozi.

Kutokana na utawala huo wa kikabila, Dkt Hailemariam Desalegn, aliyechukua uongozi baada ya kifo cha ghafla cha Meles, hakuwa na mamlaka kamili.

Alikuwa kama tarishi wa maafisa wanne wa ngazi za juu serikalini wa kabila la Tigray, miongoni mwao kiongozi wa sasa wa TPLF, Dkt Debretsion Gebremichael.

Ni kutokana na udhibiti huo ambapo vyama hivyo vilitafuta mbinu ya kujikomboa, ndiposa vikamshawishi Dkt Desalegn ajiuzulu, vikamchagua Dkt Ahmed, mwanajeshi mstaafu.

Inaaminika Dkt Ahmed alishambulia TPLF mwaka 2020 kama hatua ya mwisho ya kuhakikisha haitapumua tena ila akatoa visingizio.

Wataalamu wa vita wanahoji kwamba alinoa pakubwa kwa kuchukua hatua hiyo bila mwanzo kukadiria nguvu za TPLF.

Hatua hiyo haikutaka pupa bali mpango mzuri na taratibu ili mashambulio yakifanywa pawe na hakika ya ushindi wa haraka.

Kutokana na lile-lile tatizo la ukabila lililokita mizizi kwenye serikali ya Meles, waliokuwa majenerali wakuu wa jeshi la EPDF sasa wamo ndani ya TPLF.

Kamanda mkuu wa TPLF ni Jenerali Tsadkan Gebretensae, 68, aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Ethiopia kati ya 1991 na 2000.

Jenerali huyo anayeenziwa na mataifa ya magharibi kwa kupanga mikakati safi ya vita ndiye aliyetangaza TPLF inaelekea Addis Ababa.

Lazima Dkt Ahmed alishtuka sana!

Serikali ya Ethiopia ina afua mbili: Itafute suluhisho la kisiasa na TPLF au anga nchini humo itaharibika zaidi.

[email protected]