[ad_1]
Serikali yajitolea kuendelea kukabiliana vilivyo na magonjwa ya maeneo ya kitropiki yaliyopuuzwa
Na WANGU KANURI
HUKU serikali ikiadhimisha Siku ya Magonjwa ya Tropiki Yaliyopuuzwa (NTD) hii leo, magonjwa ya Trakoma, Matende (Elephantiasis), Upofu unaotokana na maji (River Blindness) na Kulala (Sleeping Sickness) ndiyo yanalengwa mwaka huu.
Mkuu wa Idara ya NTD, Wykcliff Omondi ameahidi kuwa magonjwa hayo manne yatakuwa yamemalizwa ifikapo 2026 huku akieleza kuwa serikali itajibidiisha kuhakikisha kuwa watadhibiti magonjwa hayo mengine kwa kupunguza maambukizi.
“Tumelenga 2026 kwa kuwa wagonjwa wanapata matibabu yanayoboresha na kukinga afya zao,” akaeleza.
Siku hii ambayo huadhimishwa duniani kote hulenga kuangazia jinsi mataifa mbalimbali yamepiga jeki katika kuhakikisha kuwa magonjwa ya NTDs yametatuliwa.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), lengo la mwaka huu ni kufikia usawa wa kiafya na kumaliza magonjwa yanayohusiana na umasikini.
Magonjwa ya NTDs huwaathiri sana kina mama na watoto wanaoishi kwenye maeneo ya joto jingi huku vifo 20,000 vikiripotiwa na watu milioni 1.9 wakiwa walemavu duniani.
Malengo ya WHO ya 2021-2030, ni kuhakikisha kuwa kupunguza idadi ya watu wanaohitaji matibabu ya NTDs kwa asilimia 90 na watu wanaokuwa walemavu kutokana na magonjwa hayo kwa asilimia 75.
Kama njia ya kumbukumbu, Dkt Omondi alieleza kuwa Kenya itawasha taa katika Jumba la Mikutano la Kenyatta (KICC) Nairobi na ngome ya Fort Jesus, Mombasa kama ishara ya umoja na mataifa yote duniani.
[ad_2]
Source link