Serikali yatakiwa itume polisi kulinda mali ya Mumias
NA SHABAN MAKOKHA
WAKULIMA na wafanyakazi wa zamani wa kampuni ya Sukari ya Mumias wanaitaka serikali kutuma maafisa wa usalama katika kiwanda cha kampuni hiyo ili kulinda mali yake kabla ya msimamizi mpya kuwasili.
Mnamo Aprili 15, Jaji wa Mahakama Kuu, Alfred Mabeya aliamuru Bw Ramana Venkata Rao aliyeteuliwa kuwa msimamizi wa kampuni hiyo kukaa kando.
Bw Kereto Marima aliteuliwa kuwa msimamizi mpya kuchukua nafasi ya Bw Rao.
Kundi la wakulima na wafanyakazi wanahofu kwamba Bw Rao, ambaye ni mkuu wa kampuni ya Sarrai Group kutoka Uganda, ambaye alipewa zabuni ya kukodisha kampuni huyo, huenda akapora mali katika kiwanda hicho.
Aidha, wanadai kuwa uporaji wa mali ya kampuni hiyo huenda ukafanyika wakati huu ambapo maafisa wa kampuni ya Sarrai wanajiandaa kuondoka.
Wakulima na wafanyakazi hao wa zamani wa kampuni ya Mumias wamemkashifu Bw Rao kwa kufeli kuweka rekodi sahihi kuhusu utendakazi wake tangu alipopewa nafasi ya kusimamia mali ya kampuni hiyo na Benki ya Kenya Commercial mnamo Septemba 2019.
Katibu Mkuu wa chama cha wafanyakazi wa kampuni hiyo Vincent Makokha alidai kuwa mwekezaji huyo amechuma Sh2.4 bilioni kutokana na uzalishaji wa ethanol tangu alipotwaa usimamizi wa kampuni hiyo.
“Hizi ni pesa nyingi kuzidi deni la Benki ya Kenya Commercial la Sh500 milioni na tunataka sehemu ya pesa zilizopatikana kutokana na uzalishaji wa ethanol zirejeshewe kampuni ya Mumias,” akasema.
Tayari, wafanyakazi wa zamani wa Mumias ambao wamepiga kambi katika nyumba za kampuni hiyo wanasema kuwa baadhi ya mashine, na gari lenye nambari ya usajili ya KBR 326Q, zilihamishwa na Sarrai Group kutoka kampuni hiyo hadi sehemu isiyojulikana.
Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi hao wa zamani Patrick Mutimba alisema visa vya kuporwa kwa mali ya kampuni ya Mumias vimekithiri zaidi.
“Hii ndiyo maana tunaitaka serikali kuwatuma maafisa wa usalama kwa kiwanda hiki ili kulinda mali ya kampuni ya Mumias. Hatuna imani na walinzi wanaolinda lango kuu la Mumias kwa sababu waliletwa na Bw Rao ambaye ametemwa kutoka Mumias,” akasema Bw Mutimba.
“Vilevile, tunataka mitambo ya kiwanda hiki ifanyiwe majaribio kubaini kama inafanya kazi kabla ya makundi haya mawili – Sarrai Group na meneja mrasimu kuruhusiwa kuondoka Mumias,” Bw Mutimba akaongeza.