Serikali yatangaza wiki ya uvumbuzi kuanzia Desemba 6
Na WANGU KANURI
SERIKALI imewaomba wavumbuzi na washauri kushiriki katika Wiki ya Uvumbuzi nchini Kenya ambayo itafanyika mnamo Desemba 6 hadi Desemba 10, 2021 katika Kenya School of Government, Lower Kabete.
Rais Uhuru Kenyatta kwenye ujumbe wake, alieleza kuwa uvumbuzi ni injini inayoendesha ujasiriamali unaofungua nafasi za ajira kwa vijana.
Isitoshe, Rais Kenyatta alisisitiza kuwa sharti washikadau wa elimu waendelee kuboresha elimu ya teknolojia ya sayansi, uvumbuzi na ujasiriamali.
Wiki hiyo ya uvumbuzi itajumuisha mikutano minne ya; uvumbuzi unaoegemea ujuzi na talanta, teknolojia na mabadiliko kwenye viwanda, biashara na uanzilishaji.
Mwenyekiti wa Agenti ya Uvumbuzi nchini (KeNIA),Dkt Tonny Omwansa akizungumza kwenye mkutano wa washikadau uliofanyika katika hoteli ya Capital Club jijini Nairobi, aliwarai wavumbuzi kuonyesha bidhaa na huduma walizounda.
“Wiki hii ya uvumbuzi itawafaa wavumbuzi na wanaweza wavutia watega-uchumi, washiriki au hata wateja. Tunawaomba wote walio na bidhaa na huduma walizovumbua waje wazionyeshe,” akasema.
Bi Sheena Raikundalia, Mkurugenzi wa Kitovu cha Teknolojia cha Uingereza nchini Kenya, alieleza kuwa wiki ya uvumbuzi itawapa motisha Wakenya ya kujishughulisha na uvumbuzi.
Hii ni baada ya kuona vitu mbali mbali vilivyovumbuliwa na wenzao.
Isitoshe, Bi Sheena alipigia debe mtaala wa CBC akisema kuwa mtaala huo utawaongoza wanafunzi katika uvumbuzi. “Uvumbuzi hulenga kusuluhisha matatizo yanayowakumba wananchi na kupanua udijitali. CBC ina mwelekeo kwa kufanikisha matakwa hayo.
“Hata hivyo, mtaala huo ili uwafae wanafunzi lazima utekelezwe kwa njia inayofaa,” akasema Bi Sheena ambaye atakuwa kiongozi wa mkutano wa ujuzi na talanta kwenye wiki ya uvumbuzi.
Mwenyekiti katika bodi ya KeNIA, Profesa Reuben Marwanga alieleza kuwa Kenya ikizidisha uvumbuzi itaweza kutajirika kwani uvumbuzi huleta huduma na bidhaa geni, nafasi za ajira na kupunguza umaskini nchini.
Wiki ya uvumbuzi itawaleta pamoja wakuu kutoka serikali za kaunti, sekta binafsi, washiriki wa maendeleo, wanahabari na jamii kwa jumla ili kuwafaa Wakenya.
Dhima ya Wiki ya Uvumbuzi ni kuonyesha uvumbuzi wa Wakenya na pia kuendeleza miradi ya nchi chini ya Ajenda Nne Kuu (Big 4 Agenda) na Ruwaza ya 2030 (Vision 2030).